Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP kushirikiana na NGOs na sekta binafsi kusambaza haraka chakula kwa wahitaji

WFP kushirikiana na NGOs na sekta binafsi kusambaza haraka chakula kwa wahitaji

Pakua

Shirika la mpango wa chakula duniani WFP hivi sasa limegeukia njia mbalimbali bunifu katika mnyororo wake wa usambazaji Afrika Mashariki na Kati kwa lengo la kuokoa na kubadili haraka maisha ya mamilioni ya watu wanaohitaji msaada. Je ni mbinu gani hizo ?.  Grace Kaneiya anatupasha zaidi

Kwa mujibu wa WFP myororo wa usambazaji ndio uti wa mgongo wa shirika hilo ambalo kila siku kwa wastani  huakikisha malori 7,500 yanakuwa barabari kwenda kusambaza chakula, ndege 92 hudondosha vifurushi vya chakula na meli 22 zinakuwa baharini zikisafirisha shehena kwa ajili ya kutoa msaada kwa watu milioni 90 kote duniani. 

Ili kuhakikisha mchakato huo unakuwa endelevu ni lazima kutumia njia ambazo zina ufanisi na za gharama nafuu. Tarek Keshavjee ni afisa wa kikanda wa masuala ya kiufundi ya WFP Nairobi Kenya amesema “WFP kila wakati inasaka mbinu bunifu ili kuboresha mnyororo wetu wa usambazaji , na katika ubunifu ni kuingia ubia na mashirika yasiyo ya kiserikali na sekta binafsi ambayo yanakuja na uzoefu mkubwa na wa jinsi gani kama WFP tunaweza kufanya vyema zaidi kazi zetu kwa kutumia ubunifu , ni katika ari ya kutaka kufikisha msaada kwa namna yeyote ile na kutoruhuru chohote kuingilia  ari hiyo.” 

Afrika Mashariki kwa mfano, WFP inashirikiana na kampuni ya nembo za biashara (East Africa Trademarks) na hivyo imepewa hadhi ya mwendeshaji wa uchumi aliyeidhinishwa ambayo imesaidia shirika hilo kuokoa muda unaotumiwa na malori ya WFP mpakani  yanaposafirisha shehena na kupunguza gharama za usafirishaji lakini pia kufikisha msaada wa chakula haraka kwa wenye njaa. 

Richard Kamajugo ni afisa mkuu wa oparesheni za East Africa Trademark , "Hii hususan ni kutokana na kutekeleza sheria na kulipa kodi mizigo inavyosafirishwa , na inamaanisha kwamba makampuni yanayofuata sheria yanalipa gharama ndogo za biashara kama zawadi, hivyo malori yanayobeba mizigo ya WFP yanapita bila usumbufu mpakani na huo ni ushidi kwa kila mtu.” 

WFP pia inaangalia njia nyingine ya ubunifu mpya kabisa wa kuanza kutumia  meli za angani  (Airship) ambazo zitapunguza gharama kwa asilimia 50 na kuweza kufikia hata maeneo yaliyo mashinani zaidi kwa urahisi , zikibeba kuanzia tani 20 hadi 500 za chakula njia ambayo itahakikisha hakuna atakayesubiri miezi au wiki kupata msaada. 

Na ubunifu mwingine shirika hilo linasema ni kutumia mashine kama za ATM za ili kutoa chakula. Hii itasaidia kupunguza gharama za usafirishaji na kuokoa muda wa wahitaji msaada kupanga foleni kungoja mgao wa kila mwezi kwani kwenye mashine hizi kwa kutumia kadi maalum wanaweza kuchukua kila siku au wakati wowote. 

Na mbinu ya mwisho bunifu ni  kutumia  teknolojia ya shamba kwenye makasha au makontena kupanda sawa na ekari kama tano za mboga na mazao mengine  kwenye makasha hayo, teknolojia ambayo inatumia maji na nishati ya jua au sola. Teknolojia hii ikifanikiwa WFP inasema inaondoa gharama zote za usafirishaji na usambazaji kwa asilimia kubwa.

Hizi ndizo baadhi ya mbinu bunifu zinazotumika na kufikiriwa kuanza kutumiwa na WFP kufanikisha operesheni zake. 

Audio Credit
Flora Nducha/Grace kaneiya
Audio Duration
3'22"
Photo Credit
WFP/Falume Bachir