Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Napenda somo la kemia, nataka kuwa daktari- Mwanafunzi Mkimbizi Sudan Kusini

Napenda somo la kemia, nataka kuwa daktari- Mwanafunzi Mkimbizi Sudan Kusini

Pakua

amishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, Filippo Grandi akiwa ziarani barani Afrika, ametembelea wanafunzi katika shule inayofanya vizuri zaidi kimasomo kwa wakimbizi na wenyeji nchini humo na akaongeza wito wa uwekezaji zaidi katika elimu kwa watu waliofurushwa na pia jamii zinazowakaribisha. Taarifa ya Grace Kaneiya inaeleza zaidi. 

Shule ya Sekondari ya Makpandu ni moja ya shule zinazofanya vizuri zaidi kimasomo nchini Sudan Kusini na inayofanya vizuri zaidi katika jimbo la Equatoria Magharibi. Ilianzishwa na UNHCR kwa kushirikiana na shirika la World Vision Sudan Kusini na pia Wizara ya Elimu ya Sudan Kusini, mnamo mwaka 2013 kwa ajili ya watoto wakimbizi na wenyeji. 

Mnamo mwaka wa 2019, wanafunzi saba wakimbizi walipata alama kati ya 10 bora katika jimbo lakini mwaka jana, janga la COVID-19 lilikatisha masomo kote nchini. Shule zilifungwa kwa miezi sita kisha zikafunguliwa mnamo Septemba ili kuruhusu wanafunzi katika mwaka wao wa mwisho wa shule ya msingi na sekondari kurudi chini ya miongozo mikali ya usalama wa afya. 

Makpandu, kambi inayohifadhi wakimbizi zaidi ya 5,000 wengi wao kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Jamhuri ya Afrika ya Kati, wanafunzi wanafanya bidii kukimbizana na muda na kujiandaa kwa ajili ya mitihani ya mwisho. 

Atovura Chantal, a mkimbizi kutoka Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, ana matamanio ya kusomea utabibu, anasema,  "Ninapenda kemia kwa sababu ikiwa kuna nafasi kwangu kuendelea na elimu yangu, ningependa kusomea udaktari ndiyo sababu ninaipenda sana." 

Wanafunzi hawa wana imani kuwa watafaulu vizuri kwenye mitihani yao ya mwisho ya shule ya sekondari lakini wana wasiwasi juu ya kile kitakachofuata kwani fursa za elimu ya juu ni chache nchini Sudan Kusini. Kwa wakimbizi, hata ni vigumu zaidi kufikia elimu ya juu. Ulimwenguni, ni asilimia 3 tu ya wakimbizi wanaoweza kupata elimu ya chuo kikuu. Atovura Chantal anatoa wito, "Wanaweza kuweka chuo kikuu kwa baadhi mahali hapa, kwa sababu tulivyo hapa kama wakimbizi, wakati mwingine, tunataka kuendelea na masomo yetu." 

Filippo Grandi, Kamishina Mkuu wa UNHCR anasema amevutiwa na uwezo wa wanafunzi hawa na anaongeza, "Ukarimu, kukaribisha wakimbizi, kuweka mipaka wazi, kama inavyofanya Sudan Kusini, sio tu nzuri kwa watu wanaokimbilia usalama, lakini inaleta fursa kwa kila mtu hapa."

Sudan Kusini ilijitenga na Sudan kuwa taifa changa zaidi ulimwenguni mnamo mwaka 2011 baada ya miongo kadhaa ya vita lakini ikatumbukia tena kwenye mzozo mnamo mwaka 2013. Zaidi ya Wasudan Kusini milioni nne wamehama makazi yao katika eneo hilo na ndani ya nchi yao katika moja ya mzozo mkubwa zaidi wa makazi nchini Afrika. 

Audio Credit
Flora Nducha/Grace kaneiya
Sauti
1'50"