Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu wasafirishwa kiharamu ili kutumikishwa kwenye kuombaomba

Watu wasafirishwa kiharamu ili kutumikishwa kwenye kuombaomba

Pakua

Idadi ya watoto wanaosafirishwa kiharamu imeongezeka mara tatu katika kipindi cha miaka 15 iliyopita, huku idadi ya wavulana kwenye kundi hilo ikiwa imeongezeka mara 5, imesema ripoti mpya ya ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kukabili uhalifu na madawa ya kulevya, UNODC. Taarifa zaidi na Assumpta Massoi.

Ripoti hiyo ya usafirishaji haramu wa binadamu duniani yam waka 2020  imezinduliwa mjini Vienna, Austria ikifafanua zaidi kuwa watoto wa kike wanasafirishwa kiharamu kwa ajili ya kutumikishwa kingono ilihali wavulana kutumikishwa kwenye ajira.

Mwaka 2018, takribani watu 50,000 walibainika na kuripotiwa katika nchi 148, ingawa ripoti hiyo inasema kwa kuzingatia kuwa biashara hiyo hufanyika kificho, idadi halisi inaweza kuwa ni kubwa. “Wasafirishaji haramu mara nyingi wanalenga watu walio na shida zaidi kama vile wahamiaji na wale wasio na ajira. Janga la COVID-19 limechochea mdororo wa kiuchumi na hivyo kuweka zaidi watu kwenye hatari ya kutumbukia kwenye mtego wa kusafirishwa kiharamu,” imesema ripoti hiyo.
Akizungumzia ripoti hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa UNODC Ghada Waly amesema, “mamilioni ya wanawake, wanaume na watoto duniani kote hawana kazi, hawako shuleni, na hawana msaada wa kijamii wakati huu ambapo janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 linaendelea kutikisa duniani na hivyo kuwaweka hatarini kusafirishwa kiharamu. Tunahitaji hatua mahsusi za kuzuia wasafirishaji haramu wasitumie shida za wengine kujinufaisha.”
Ripoti hiyo inalenga kupatiwa serikali hatua za kuchukua kukabili usafirishaji haramu, sambamba na kuhakikisha hakuna anayekwepa sheria na kusaidia manusura wa vitendo hivyo kama sehemu za kuondokana na vitendo vya usafirishaji haramu wa binadamu.
Ripoti inaonesha kwamba wanawake wameendelea kuwa waathirika wakuu wa biashara hiyo ambapo katika kila watu 10 waliosafirishwa kiharamu duniani mwaka 2018, wanawake ni watano na wasichana ni wawili. Asilimia 20 ya waathirika kwa mujibu wa takwimu hizo walikuwa ni wanaume na asilimia 15 wavulana.
Asilimia 50 ya waliosafirishwa kiharamu walilengwa kutumikishwa kwenye ngono, asilimia 38 kutumikishwa kwenye ajira ilihali asilimia sita walitumikishwa kwenye vitendo vya uhalifu. Asilimia moja walitumikishwa kuombaomba na wengine kwenye ndoa za lazima, kutoa viungo vyao vya ndani na maeneo mengine.
Hivi sasa wasafirishaji hao haramu wa binadamu wanatumia teknolojia za kisasa kuanzia mchakato wa kupata watu, kuwaajiri hadi kuwatumikisha. “Idadi kubwa ya watoto wanafuatwa kupitia mitandao ya kijamii kwa kuwa ni rahisi kuwafikia na kuwarubuni na wao watoto kukubali kupitia mbinu mbalimbali ikiwemo kuwaomba urafiki. UNODC imebaini njia mbili moja kuwawinda mitandaoni na pili kutangaza matangazo na kusubiri watu kujibu.”
Ripoti ya dunia kuhusu usafirishaji haramu wa binadamu hutolewa na UNODC kila baada ya miaka miwili kuhabarisha kuhusu hatua bora za kukabili uhalifu huo kwa kuzingatia ajenda 2030 au malengo ya maendeleo endelevu, SDGs ya Umoja wa Mataifa.
Takwimu za mwaka huu zinatoka mataifa 148 na inachunguza kesi 489 za mahakamani kutoka nchi 71.
 

Audio Credit
Flora Nducha/Assumpta massoi
Audio Duration
3'8"
Photo Credit
UN