Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi wa UN umenusuru watoto wetu na ndoa za umri mdogo- Wazazi Tanzania

Mradi wa UN umenusuru watoto wetu na ndoa za umri mdogo- Wazazi Tanzania

Pakua

Wazazi nchini Tanzania wameupokea vizuri mradi unaotekelezwa na mashirika matatu ya Umoja wa Mataifa, lile la elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO, la masuala ya idadi ya UNFPA na la wanawake UN Women, ambao unalenga kuwawezesha wasichana kupitia elimu. Baada ya jana kuwaangazia wasichana wanufaika wa mradi huu, leo, Ahimidiwe Olotu ametuandalia sehemu ya pili inayoangazia wazazi na wanajamii kwa ujumla.   

Huyo ni Amani George, Mwalimu na pia Mratibu wa kikundi cha vijana katika shule ya Sekondari Ngweli, iliyoko Sengerema Tanzania. Mwalimu George anaongeza, "wanaomaliza, hasa kidato cha nne, wanaondoka na elimu hii ya ujasiriamali, hivyo inaweza kuwasaidia hata wakiwa maisha ya mbali na shule. Kwa hiyo wanaweza kutoka elimu ya ujasiriamali na kuanzisha miradi midogomidogo.” 

Mwingine, ni Mwalimu Neema Zakaria, yeye anaeleza mchango wa wazazi katika kufanikisha miradi kama hii, 

“Tunajitahidi kupata ushirikiano na wazazi. Tunawaeleza mambo kama haya, ni mambo gani wawafanyie watoto, hasa wanaofanyiwa ukatili hasa huko nyumbani. Watoto wa kike, wakiume wawatendeeje, utaangalia jinsi gani watoto wanaweza wakawa salama katika maeneo fulani fulani.” 

Mohamed Khamis, ni mzazi ambaye binti yake Fatma alipata changamoto zilizomfanya kushindwa kumaliza kidato cha nne, lakini sasa mradi huu umemsaidia msichana huyo kujifunza ufundi, kusoma na kuandika na ujasiriamali. Mzee Khamis anasema, 

“Wengi wakishakataa, wanasubiri tu mume. Lakini hili lilipokuja, naona kidogo kuna matumaini mengine ya kimaisha.”  

Asela Mataba, ni mama wa msichana Angel ambaye yeye sasa yuko kidato cha nne. Mama huyu anaeleza kwa nini anaona mradi huu ni wa manufaa makubwa, 

"Mtoto wa kike asipokuwa na uelewa, asipokuwa na kazi, asipoweza kujiamini, asipoweza kusimama yeye mwenyewe, akatembea yeye mwenyewe, inakuwa ni ngumu sana katika maisha yake.” 

Ni wazi kwa maoni hayo, wazazi wameupokea mradi huu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa kama anavyoeleza Abdallah Omar, kiongozi wa kijamii, "kwa kuwa wazazi waliupokea huu mradi, na wakakubali watoto wao washiriki huu mradi, ni kusema kwamba huu mradi, umepokelewa vizuri ndani ya jamii.” 

Audio Credit
Flora Nducha/Ahimidiwe Olotu
Audio Duration
2'38"
Photo Credit
UN News