Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tujikwamue kwa pamoja 2021 dhidi ya COVID-19- Guterres

Tujikwamue kwa pamoja 2021 dhidi ya COVID-19- Guterres

Pakua

Mwaka 2020 ulikuwa ni mwaka wa majanga lakini 2021 ni mwaka wa fursa na matumaini! Ni kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliyotoa leo kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa akielezea vipaumbele vyake 10 kwa mwaka 2021. Assumpta Massoi na maelezo zaidi. 

Guterres akianza hotuba yake kwa lugha ya kilatini, Annus Horribilis kwa 2020 na annus possibilitatis kwa mwaka 2021 amesema mwaka 2020 ulikuwa wa kifo, janga na kukata tamaa. 

Amesema, “Tumepoteza watu milioni 2, wakiwemo wanafamilia ya Umoja wa Mataifa. Idadi ya vifo inaongezeka, gharama za kiuchumi halikadhalika. Ajira milioni 500 zimepotea. Umasikini wa kupindukia umerejea katika viwango havijawahi kushuhudia katika vizazi kadhaa. Pengo la ukosefu wa usawa linaongezeka. Njaa inaongezeka tena. Utete kwenye dunia umefichuka. Tumetangaza vita dhidi ya mazingira na mazingira yanajibu. Janga la tabianchi linasambaa.”  

 Bwana Guterres amesema pamoja na changamoto zote hizo, mwaka 2021 lazima uwe mwaka wa kubadilisha mbinu na kurejesha dunia kwenye mwelekeo sahihi na ametaja vipaumbele vyake 10 atakavyozingatia kwa mwaka huu wa 2021. 

 Vipaumbele hivyo ni kusongesha usawa katika chanjo dhidi ya COVID-19, kujikwamua kutoka COVID-19 kupitia mbinu endelevu na zisizoharibu mazingira, hatua kwa tabianchi, kukabili ukosefu wa usawa na umaskini, haki za binadamu, usawa wa jinsia, amani, usalama na sitisho la mapigano, kutoendeleza nyuklia, ukiritimba katika teknolojia za digitali na kupanga upya ajenda ya dunia kwa ustawi wa wote. 

 Mathalani kwenye Chanjo dhidi ya COVID-19 amesema janga la Corona katu haliwezi kumalizwa na nchi moja pekee,

“Iwapo virusi hivyo vitaachiwa visambae kama moto wa nyika katika nchi za kusini, vitabadilika tabia zao na kuweza kusambaa kwa haraka zaidi, kusababisha vifo na kuwa sugu kwa chanjo na kisha kurejea katika nchi za kaskazini.” 

Amesema cha kusikitisha zaidi chanjo zinafikia haraka nchi chache ilhali nchi masikini zaidi hazina kabisa chanjo hizo. “Sayansi inafanikiwa lakini mshikamano unashindikana.” 

Bwana Guterres amesema katika mazingira kama hayo, mshindi pekee katika dunia ya walio nacho na wasio nacho ni virusi! 

Guterres amesema wakati  huu ambapo dunia inahaha kujikwamua kutoka janga la COVID-19,  mikakati ya kukwamuka huko lazima iwe jumuishi na endelevu na ni lazima ianze kuandaliwa sasa kwa kuwa dunia haiwezi kusubiri kuponyeka kutoka kwenye janga la Corona iwapo uchumi uko mahututi. 

Ni kwa mantiki hiyo amesema kinachohitajika ni uwekezaji mkubwa katika mifumo ya afya kila pahali, huduma ya afya kwa kila mtu, au UHC, afya ya akili ipatiwe kipaumbele, hifadhi ya jamii kwa kila mtu, ajira zenye hadhi, watoto warejee shuleni salama na zaidi ya yote nchi tajiri ziangalie uwezekano wa kufuta madeni ya nchi maskini kwa kuwa hivi sasa shughuli za kiuchumi zimedumaa. 

 

 

Audio Credit
Flora Nducha/Assumpta massoi
Sauti
3'2"
Photo Credit
UNICEF Malawi Video capture