Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNIDO yasaidia kunoa stadi za vijana katika ujasiriamali

UNIDO yasaidia kunoa stadi za vijana katika ujasiriamali

Pakua

Shirika la Umoja wa Mataifa la maendeleo ya viwanda UNIDO limesema vijana wanachokihitaji ni nyenzo, mbinu na muongozo ili kujenga kesho wanayoihitaji na hasa kupitia ujasiriliamali. Maelezo John Kibego yanafafanua.

Kwa mujibu wa taarifa ya UNIDO iliyotolewa mapema wiki hii ikiangazia umuhimu wa vijana kubadilika "kutoka kuwa wasaka ajira na kuwa waunda ajira,"  ubunifu na mtazamo wa ujasiriliamali utawasaidia vijana kufanya mabadiliko yanayohitajika na wataweza kuchangia katika mustakbali ambao ni jumuishi na endelevu. 

Shirika hilo la maendeleo ya viwanda limesema katika nchi nyingi asilimia 70 ya watu ni vijana wengi wakiwa wa chini ya umri wa miaka 30 na kwa kutambua hilo, UNIDO imeanzisha programu maalum za kuwasaidia vijana kufikia uwezo wao kupitia shughuli za ujasiriliamali katika nchi mbalimbali duniani. 

Kwani shirika hilo linasema serikali haziwezi kumudu tena mzigo mkubwa wa vijana wasio na ajira na lengo ni kuhakikisha vijana wanachangia katika kutatua changamoto kubwa zinazoikabili jamii kama  vile uhakika wa chakula, ukosefu wa ajira, uhamiaji na usalama. 

UNIDO imesisitiza kwamba "hayo ni muhimu katika kuhakikisha mustakbali bora wa vijana na jamii kwa ujumla. "

Shirika hilo linasema ili kufikia malengo hayo kupitia mkakati wa Umoja wa Mataifa wa ajenda ya maendeleo ya 2030 kwa vijana, limeweka mahitaji ya kundi hilo katika kitovu cha shughuli zake kuhakikisha kuna maendeleo jumuishi na endelevu ya viwanda au (ISID). 

Kwa kushirikiana na sekta za umma na binafsi UNIDO inato msaada wa kiufundi ambao unawasaidia vijana kutotegemea kuajiriwa na badala yake kupata ujuzi na kuanza kujiajiri kupitia masomo ya nadharia na ya vitendo. 

Na mafunzo haya yanawasaidia wavulana na wasicha kujijengea uwezo kutokana na ujuzi wanaoupata na hivyo kujenga kizazi cha wajasiriamali wanaojiajiri na sio wanaotegemea kuajiriwa. 

Miongoni mwa wadau wakubwa katika program hizo za UNIDO ni makampuni ya kimataifa kama Scandia, Komatsu, lakini pia  serikali za Japan, Sweden na mashirika mengine. 

Audio Credit
Flora Nducha/John Kibego
Audio Duration
1'54"
Photo Credit
UN Environment/Georgina Smith