Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sasa hatuonji tena maji, tunatumia simu za kiganjani- Wakulima wa mpunga Vietnam

Sasa hatuonji tena maji, tunatumia simu za kiganjani- Wakulima wa mpunga Vietnam

Pakua

Nchini Vietnam, mfuko wa maendeleo ya Umoja wa Mataifa, IFAD umesaidia wakulima kuondokana na tabia ya kuonja maji ya umwagiliaji ili kutambua kiwango cha chumvi na badala yake sasa wanatumia teknolojia ya simu ya kiganjani ili kuongeza mavuno ya mpunga. Assumpta Massoi na maelezo zaidi.

Simu za kiganjani zimekuwa mkombozi kwenye kilimo kuanzia Kenya, Bolivia hadi Cambodia ambapo teknolojia ziwe za kuuza bidhaa au kutambua hali ya hewa zimesaidia mathalani wakulima na wavuvi kutambua msimu wa mavuno, uvuvi au upanzi. 

Nchini Vietnam, wakulima wa mpunga wamekuwa wakihaha kutambua ni vipi wanaweza kuongeza kiwango cha mavuno yao hasa kwa vile wanatumia mfumo wa umwagiliaji. 

Thach Thi Than ni mkulima katika jimbo la Tra Vinh na anasema “pindi maji yenye chumvi yanapoingia shambani, huathiri mpunga na hata kuua mpunga wote. Mathalani msimu uliopita, shamba letu la mpunga liliharibika. Kwa kawaida tunapata magunia 16 ya mpunga kwa ekari moja lakini kwa sababu ya kiwango kikubwa cha chumvi kwenye maji tunapata magunia 5 hadi 6. Kwa hiyo chumvi inatuathiri sana.” 

Kilio chao kimesikika na kampuni ya RYNAN imekuja na teknolojia ya kuweka kifaa shambani na kusoma kiwango cha chumvi na matokeo yake kuoneshwa kwenye simu ya kiganjani. Huynh Nghia Tho ni kutoka IFAD ni Meneja wa mradi. “Kila dakika 15, sampuli ya maji inachukuliwa na taarifa zinapelekwa kwenye kituo cha operesheni, zinachambuliwa kiwango cha chumvi,uwezo wa maji kukabili aside na hata kiwango cha mawimbi ya maji. Na hatimaye wakulima wanapatiwa taarifa kupitia apu iliyoko kwenye simu.” 

Kwa Thach Thi Than, haya ni mapinduzi ya kilimo kwa kuwa anasema, “zamani, wazazi wetu walipotaka kutambua iwapo maij yana chumvi au la, waliyaonja ili hatimaye waamue kuyafungulia kwenye shamba au la. Lakini sasa tunaweza kusalia nyumbani na kuweza kupata taarifa za kiwango cha chumvi kwenye maji.” 

Nguyeni Thi Lun, afisa kutoka Idara ya maendeleo ya kilimo vijijini nchini Vietnam anasema hatua hii ni mujarabu kwa kuwa kipimo kinasaidia watu kupunguza hatari ya kufungulia maji ya chumvi kwenye mashamba yao ya mpunga na hivyo kuongeza uzalishaji. 

Miradi kama hiyo inatekelezwa wakati huu ambapo IFAD imetambua umuhimu wake na imezindua mpango wa dola milioni 500 wa kusaidia wakulima kufuata kilimo cha kisasa na kinachohimili mabadiliko ya tabianchi, ASAP+, ikiwa ni mradi wenye fedha nyingi zaidi kwa lengo la kusaidia wakulima wadogo. 

Hivi sasa ni asilimia 1.7 ya fedha  kwenye mfuko wa mabadiliko ya tabianchi ndio zinafikia wakulima wadogo. 

Audio Credit
Flora Nducha/Assumpta massoi
Audio Duration
2'49"
Photo Credit
UN