Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashirika ya UN yasaidia ujenzi wa mwalo huko Galmudug, Somalia

Mashirika ya UN yasaidia ujenzi wa mwalo huko Galmudug, Somalia

Pakua

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa umeendelea na mfululizo wa ziara zake katika majimbo yanayounda serikali ya shirikisho, Somalia. Ujumbe huo ukiongozwa na Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na ambaye pia ni Mkuu wa mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia UNSOM, Bwana James Swan, wametembelea jimbo la Galmudug kujadiliana na uongozi jinsi Umoja wa Mataifa unavyoweza kusaidiana nao. Ahimidiwe Olotu na maelezo zaidi. 

Bwana Swan na maafisa wengine wa Umoja wa Mataifa, kwa njia ya Helikopta wanalikata anga kuelekea katika Jimbo la Galmudug, katikati mwa Somalia ambako watakutana na viongozi wa Jimbo wakiongozwa na Rais wa Jimbo hilo Ahmed Abdi Kariye. Mkutano wao na viongozi hawa unafanyika katika mji mkuu wa jimbo hilo, Dhusamareb.  

Katika mkutano wa pamoja wa viongozi hawa, Bwana Swan anaeleza mifano kadhaa ya kazi ambazo zinafanywa na mashirika ya Umoja wa Mataifa kuisadia Galmudug.  Kazi hizo ni pamoja na msaada kutoka WFP kwa ufadhili wa serikali ya Italia pia kwa kushirikiana na mamlaka za jimbo katika kujenga mwalo katika wilaya ya Hobyo ambao utasaidia kuegesha boti za uvuvi.  

Mradi huu ulianza mwezi Desemba mwaka jana 2020, lengo la mradi ni kusaidia kuamsha shughuli ya  uvuvi za hapa, pia kuwezesha usafirishaji nje ya hapa mara tu mradi utakapomalizika katika msimu kiangazi wa mwaka huu. Zaidi ya ujenzi, WFP pia inafundisha jamii ustadi mpya wa uvuvi na mbinu za uhifadhi, kwa kushirikiana na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali. 

Mradi huo ni nyongeza katika mpango wa msingi wa WFP wa kutoa chakula, fedha taslimu na vocha kwa watu takribani 300,000 wenye uhitaji kila mwezi kote Galmudug. Bwana Swan amesema kuwa inatarajiwa kwamba misaada hii ya kibinadamu itaongezwa mwaka huu. 

Pia Bwana Swan ameeleza shughuli za shirika la UNDP ambalo pamoja na mambo mengine limesaidia katika masuala ya utawala kwa kuwapa mafunzo mbalimbali maafisa wa serikali.  

(Sauti ya Swan) – KIBEGO 

"Msaada UNDP pia umejumuisha kuwezesha ushiriki wa zaidi ya maafisa wa serikali 1,000, wawakilishi wa asasi za kiraia, wazee, wanawake na viongozi wa vijana katika mikutano inayohusiana na maridhiano, mashauriano na warsha." 

Majadiliano ya Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na rais wa Galmudug pia yamegusia hali pana ya kisiasa nchini Somalia, hasa matayarisho ya uchaguzi na umuhimu wa kusuluhisha masuala yenye utata ili mchakato wa uchaguzi unaofaa uweze kufanyika kote nchini mwezi ujao. Swan anasema,  

(Sauti ya Swan) - KIBEGO 

"Tunawahimiza viongozi wote wa Somalia kufanya kila juhudi kushiriki katika mazungumzo katika roho ya udugu ili uchaguzi wa kitaifa ufanyike kwa msingi wa makubaliano mapana, yaliyotokana na Mkataba wa Septemba 17, na unaungwa mkono na uwazi, haki na ujumuishaji." 

Audio Credit
Flora Nducha/Ahimidiwe Olotu
Audio Duration
1'49"
Photo Credit
UN / Omar Abdisalan