Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukisikia kuruka maji kukanyaga moto ndio kiwakutacho wakimbizi kutoka Burkina Faso

Ukisikia kuruka maji kukanyaga moto ndio kiwakutacho wakimbizi kutoka Burkina Faso

Pakua

Nchini Burkina Faso, watu waliofurushwa katika makazi yao, wanahangaika kutafuta kimbilio dhidi ya vurugu na athari za mabadiliko ya tabianchi. Baada ya kuacha nyumba zao, ambako ukame umekuwa wa kawaida, maelfu ya watu wakati huo huo wanakabiliwa na mafuriko makali ambayo yalifuta makazi yao.

Katika eneo la Sahel lenye machafuko barani Afrika, Burkina Faso iko katika kitovu cha mojawapo ya mzozo unaokua kwa kasi zaidi ulimwenguni. Mtu mmoja kati ya kila watu 20 ambayo ni sawa na zaidi ya watu milioni moja sasa amehama makazi yake. Burkina Faso pia inahifadhi wakimbizi 20,000 wa Mali, ambao wengi wao walitoroka vurugu mnamo mwaka 2012. Huyu ni mkulima aliyefurushwa anasema, “Jina langu ni Sayoré Dramane. Niliondoka kwenye nyumba yangu kwasababu ya kukosekana kwa usalama. Magaidi walikuja katika kijiji changu na kuanza kuua watu. Ndio maana tukaja hapa Kongoussi.” 

Sayore akiwa na mkewe na watoto wao wanne, alitafuta usalama katika eneo jingine humo humo Burkina Faso akayatelekeza mazao yake ili aiokoe familia. Aliona ukulima ukiendelea kuwa mgumu kwa kadri eneo la Sahel lilivyozidi kuwa kame. (Nats) Sayore anaongeza kusema kuwa, "ni kwa sababu ya ukosefu wa mvua, na jangwa, kwa sababu watu wanakata miti, na hii inaongeza joto katika tabianchi.”  

Sayore anaweza hata kufikia kufikiri kuwa ng’ombe wa maskini hazai kwani athari za mabadiliko yabianchi zimemfuata hapa Kongoussi alipokimbilia. Mwaka jana, makazi yake yalisombwa na mafuriko ambayo yaliharibu nyumba za zaidi ya familia 1,700 zilizofurushwa katika eneo hilo. 

Thierry Zinta Thianhoun, ni Ofisa wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR anasema,  “Mabadiliko ya ya tabianchi yamezidisha tishio. Katika muktadha huu, haishangazi, tunaona mzozo juu ya shamba, migogoro juu ya ardhi ya malisho na upatikanaji wa maji, na pia athari zake kwenye mzozo kati ya jamii na masuala ya usalama. " 

UNHCR na wadau wanafanyia kazi suluhisho endelevu na kuimarisha msaada kwa wenyeji na watu walioyakimbia makazi yao.  

Audio Credit
Flora Nducha/John Kibego
Audio Duration
1'58"
Photo Credit
WFP/Mahamady Ouedraogo