Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ndizi zageuzwa unga huko Nyeri na sasa vijana wajipatia kipato- IFAD

Ndizi zageuzwa unga huko Nyeri na sasa vijana wajipatia kipato- IFAD

Pakua

Chukua vijana wajasiriamali, wapatie vifaa vya kisasa na mafunzo basi utakuwa umebadilisha maisha si ya kwao tu bali na jamii zao ,na hicho ndio kilichotokea huko Nyeri nchini Kenya baada ya Umoja wa Mataifa na serikali ya Kenya kushikana mikono na kunasua vijana ambao walikuwa kidoto wakate tamaa. Grace Kaneiya anasimulia zaidi. 

Eneo la Nyeri nchini Kenya, vijana 15 wakiwa katika eneo lao la kusindika ndizi kuwa unga wenye ubora.  

Leo wanaonekana na heka heka, lakini mwaka jana janga la Corona au COVID-19 liliwalazimu kufunga kiwanda chao hiki kwa miezi minne.  

Baada ya kubonga bongo, vijana hawa wakageukia mitandao yao ya kijamii kusaka masoko ya bidhaa zao kama asemavyo Joyce Murithi Gatongo, mwanachama wa G-Start. 

(Sauti ya Joyce Gatongo) 

Kuna akaunti ya Facebook, hiyo tunatumia sana kuuza bidhaa, na pia kuna video tumeweka video Youtube.” 

Kupitia mitandao ya kijamii, wateja walianza kuulizia bidhaa na hivyo G-Start wakaanza kupelekea wateja bidhaa majumbani. 

Wazo la G-Start lilitokana na Charles Mwangi mwaka 2013 baada ya kuona vijana kutoka familia za wakulima walikuwa wanahaha kujinasua kutoka kwenye umaskini. 

Charles anasema, « Tulianzisha G-Start ili kusaidia wakulima wetu ambao wengine ni wazazi wetu na baadhi waliuza mazao yao kama ndizi kwa bei ya chini. hivyo tuliamua kufanya kitu kama vijana ili tusaidie jamii. » 

Uhaba wa mashine za kisasa na mbinu bora za kusindika mazao vilikwamisha ndoto yao kwa miaka 6, hadi mwaka jana shirika la maendeleo ya kilimo la Umoja wa Mataifa, IFAD na serikali ya Kenya waliwapatia mafunzo na vifaa vya kisasa na eneo la kusindika na sasa kasi ya uzalishaji imeongezeka na jamii inawaheshimu. 

Zaidi ya yote wamepata wateja wapya kutoka maeneo mbalimbali ya Kenya. Joyce anasema, 

(Sauti ya Joyce Githongo) 

“Vile nawaambia vijana ni kwamba waache uoga na wakabiliane na maisha na wawe wavumilivu, si kwamba unaanza biashara na kupata fedha papo hapo, unaweza kuanguka lakini siku moja utafaidika.” 

Ndoto ya G-Start mwakani ni kuanza kutengeneza mvinyo wa ndizi na hata kufungua duka la kuoka mikate kwa kutumia unga wa ndizi. 

Audio Credit
Flora Nducha/Grace kaneiya
Audio Duration
2'19"
Photo Credit
FAO