Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi wazee Afrika hatarini zaidi kuathiriwa na COVID-19

Wakimbizi wazee Afrika hatarini zaidi kuathiriwa na COVID-19

Pakua

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limeonya kwamba zaidi ya wazee 500,000 barani Afrika wako hatarini kupata virusi vya Corona au COVID-19 endapo hatua madhubuti hazitachukuliwe sasa na wadau wote kuwalinda. Tupate maelezo zaidi na Jason Nyakundi 

Kwa mujibu wa shirika hilo wengi wa wazee hao wakimbizi hawana fursa za kutosha za kupata huduma za msingi kama maji, afya na vifaa vya usafi na kujisafi hali inayowaweka hatarini zaidi na hivyo wanahitaji msaada wa haraka kuweza kulindwa dhidi ya janga la COVID-19 ambalo hadi sasa limeshakatili maisha ya watu zaidi ya milioni mbili duniani kote. 

UNHCR imeongeza kuwa barani Afrika wazee wanathaminiwa na jamii zao na wengi ni babu, nyanya, mama, baba, wajomba na shangazi katika jamii hizo na wanaleta furaha, upendo, hekima na busara zinazotegemewa na wengi. Betty Sandi mkimbizi kutoka Sudan anaishi kambini Uganda na nyanya yake anayempenda  sana akisema, “Ninapopata chakula nabakisha kiasi kwa ajili ya nyanya yangu, nitafanya lolote niwezalo kwa ajili yake” 

Takwimu za shirika hilo la wakimbizi zinaonyesha kuwa kuna zaidi ya wazee 500,000 ambao ni wakimbizi na waomba hifadhi Afrika na ni miongoni mwa makundi yaliyo hatarini zaidi kuambukizwa virusi vya corona na kusahaulika. Fadou kutoka Somalia ni mmoja wa wazee hao wakimbizi na anaishi kwenye kambi ya wakimbizi ya Kakuma nchini Kenya anasema“Natumai na kuomba kwamba Mungu atatulinda na kutuepusha dhidi ya gonjwa hili na kutupa amani”. 

UNHCR inasisitiza kwamba sasa kinachohitajika ni hatua za haraka ili kulinda na kuokoa maisha ya ajuza hawa ambao ni urithi na lulu ya Afrika. 

Audio Credit
Flora Nducha/ Jason Nyakundi
Sauti
1'42"
Photo Credit
World Bank/ Eric Miller