Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chonde chonde tusaidie wakazi wa Cabo Delgado- UN

Chonde chonde tusaidie wakazi wa Cabo Delgado- UN

Pakua

Umoja wa Mataifa umeelezea wasiwasi wake mkubwa kuhusu kuendelea kuzorota kwa hali ya kibinadamu na kuongezeka kwa ghasia katika jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji. Grace Kaneiya na maelezo zaidi.

Wakurugenzi wa kikanda wa mashirika ya Umoja wa Mataifa kwa ukanda wa Kusini na Mashariki mwa Afrika wameelezea wasiwasi wao huo hii leo kupitia taarifa yao ya pamoja iliyotolewa mjini Johannesburg nchini Afrika Kusini.
Wameema ghasia zinazoendelea zimefurusha maelfu ya watu makwao na kutegemea zaidi misaada ya kibinadamu.
“Kwa mujibu wa serikali ya Msumbiji, vikundi vilivyojihami vimefanya mashambulizi na kulazimu watu zaidi ya 565,000 kukimbia vijiji vyao na kuacha mazao shambani na vyanzo vyao vya kujipatia kipato,”  imesema taarifa hiyo.
Mwezi uliopita wa Desemba, wakurugenzi hao walitembelea Msumbiji kutathmini hali halisi na mahitaji ya wakazi wa eneo hilo na jamii zinazowahifadhi huko Cabo Delgado na pia kukutana na maafisa wa serikali. 
Walieleza hofu yao kubwa juu ya kuendelea kuibuka kwa janga la kibinadamu ambako wananchi wanakumbwa pia na vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu na pia wanakosa huduma muhimu ikiwemo chakula.
Hali ya usalama inavyozidi kudorora na miundombinu kuzidi kuharibika inamaanisha inakuwa vigumu kufikia wananchi na janga la COVID-19 limefanya hali kuwa mbaya zaidi.
Wakati msimu mwingine wa mvua unatarajiwa hivi karibuni, viongozi hao wamesema madhara ya vimbunga Idai na Kenneth ni kumbusho kuwa eneo hilo liko hatarini tena kupigwa na madhara ya mabadiliko ya tabianchi.
Janga la Corona nalo limesababisha shule kuendelea kufungwa, na hivyo viongozi hao wametilia shaka uwezekano wa uwekezaji wa dhati wa kijamii kwenye elimu na nguvu kazi.
Wametaka hatua za dharura za ulinzi kwa jamii hizo sambamba na huduma muhimu kama vile chakula, afya, lishe bora kwa watoto na wanawake walioko hatarini pamoja na chanjo na huduma za ushauri nasaha na kupatia uwezo wakimbizi wavuvi na wakulima kuweza kurejea katika shughuli zao za kujipatia kipato.
 

Audio Credit
Flora Nducha/Grace kaneiya
Audio Duration
2'2"
Photo Credit
UNICEF/Mauricio Bisol