Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuwepo kwa hifadhi ya chanjo kutarahisisha vita dhidi ya milipuko ya Ebola:UN

Kuwepo kwa hifadhi ya chanjo kutarahisisha vita dhidi ya milipuko ya Ebola:UN

Hifadhi ya chanjo ya Ebola kwa ajili ya kusubiri wakati wa dharura yaanzishwa 

Kupitia taarifa iliyotolewa hii leo New York Marekani na Geneva Uswisi, mashirika manne ya kimataifa ya afya na misaada ya kibinadamu yametangaza kuanzishwa kwa hifadhi ya chanjo ya Ebola ulimwenguni ili kuhakikisha upatikanaji wa chanjo kwa haraka pindi panapotokea mlipuko wa ugonjwa huo hatari. Taarifa ya Ahimidiwe Olotu na ina maelezo zaidi. 

(Taarifa ya Ahimidiwe Olotu) 

Juhudi za kuanzisha hifadhi zimeongozwa na Kikundi cha kimataifa cha uratibu kuhusu utoaji wa chanjo, ICG ambacho ambacho kinaundwa na  Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa, WHO, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Msalaba na Hilal nyekundu, IFRC, Madaktari wasio na mipaka, MSF, kwa msaada wa kifedha kutoka kwa muungano wa chanjo duniani, Gavi. Hifadhi hiyo itaruhusu nchi, kwa msaada wa mashirika ya kibinadamu, kupambana na milipuko ijayo ya Ebola kwa kuhakikisha upatikanaji wa chanjo kwa watu walio katika hatari wakati wa milipuko. 

Chanjo ya ebola ya dozi moja ya sindano rVSV∆G-ZEBOV-GP imetengenezwa na Merck, Sharp & Dohme (MSD) Corp na im kwa msaada wa kifedha kutoka  serikali ya Marekani. Shirika la Dawa la Ulaya liliipatia leseni chanjo ya Ebola mnamo Novemba 2019, na chanjo hiyo sasa imepewa sifa za awali kutumika na WHO, na imepewa leseni na Mamlaka ya Chakula na Dawa ya Marekani na pia katika nchi nane za Afrika. 

Taarifa hiyo imeeleza kuwa chanjo hiyo kabla ya kupata leseni, ilijaribiwa kwa watu zaidi ya 350,000 nchini Guinea na katika milipuko ya Ebola ya 2018-2020 katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC chini ya itifaki ya majaribio.  

Chanjo, ambayo inapendekezwa na Jopo la ushauri wa kimkakati kwa Shirika la Afya Duniani WHO kuhusu masuala ya chanjo, SAGE inakinga dhidi ya aina ya virusi vinavyofahamika kama Zaire ebolavirus ambavyo vinajulikana sana kusababisha milipuko ya ebola. 

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt Tedros Ghebreyesus anasema, “janga la COVID-19 linatukumbusha nguvu ya ajabu ya chanjo kuokoa maisha dhidi ya virusi hatari. Chanjo za Ebola zimefanya moja ya magonjwa yanayoogopwa zaidi duniani, kuzuilika. Hifadhi hii mpya ya chanjo ni mfano bora wa mshikamano, sayansi na ushirikiano kati ya mashirika ya kimataifa na sekta binafsi katika kuokoa maisha.” 

Hifadhi hiyo ya chanjo ambayo itakuwa chini ya UNICEF imehifadhiwa nchini Uswisi na iko tayari kusafirishwa kwenda nchi mbalimbali wakati wa dharura kulingana na maamuzi yatakayofanywa na kikundi cha kimataifa cha uratibu wa chanjo. Uamuzi wa kupeleka chanjo mahali utafanywa ndani ya saa 48 baada ya kupokea ombi kutoka kwa nchi husika. Mpango ni kuwa, chanjo iweze kuifikia nchi husika ndani ya siku saba.  

Audio Credit
UN News/ Ahimidiwe Olottu-UNIC Dar
Photo Credit
Shirikisho la vyama vya msalaba mwekundu na hilal nyekundu