Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

NIlisaidiwa , sasa ni wakati wangu kusaidia :Liberee

NIlisaidiwa , sasa ni wakati wangu kusaidia :Liberee

Pakua

Wahenga walinena ukishikwa shikamana, na ndivyo anavyofanya Liberee Kayumba ambaye ni manusura wa mauaji ya kimbari ya Rwanda dhidi ya Watutsi yaliyofanyika mwaka 1994, anasema yuko hai leo hii sababu ya msaada wa chakula wa shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula WFP , ambao ulimuhamasisha baadaye kujiunga na shirika hilo kusaidia wakimbizi wa Burundi kama alivyosaidiwa. John Kibego anasimulia zaidi 

(TAARIFA YA JOHN KIBEGO) 

Liberee ameshuhudia madhila ya vita kwa macho yake, kwani alipokuwa na umri wa miaka 12 tu alipopoteza wazazi wake wote na kaka zake kwenye mauaji  ya kimbari na kuwa kwenye hatari kubwa ya kufa njaa.  Anasema “Kwa miezi mitatu nilikuwa ndani tu ya nyumba bila kujua kama ntaishi ama nitakufa saa yoyote, hakuna hata mtu mmoja kwenye familia aliyeweza kutoka nje wakati huo kwenda kufanya kazi au kulima hivyo kupata chakula ilikuwa vigumu, tusingeweza kuishi bila msaada wa kibinadamu wa chakula wa WFP” 

Na msaada huo ndio uliokuwa hamasa kwake kujiunga na WFP ili asaidie kuleta mabadiliko kwenye maisha ya wengine wanaopitia madhila aliyowahi kuyaonja. 

Hivi sasa ni afisa mwangalizi wa WFP kwenye kambi ya wakimbizi ya Mahama, iliyoko kilometa chache kutoka mpaka wa Tanzania ambayo inatoa msaada wa mgao wa chakula kila mwezi kwa karibu wakimbizi 60,000 wa Burundi. 

Liberee anaongeza kuwa “tangu nilipokuwa mtoto nilipenda kusaidia wenye uhitaji, inakutia moyo kufanya hivyo unaposhuhudia watu wakiua watu wengine na madhila yote yanayotokea. Kumbukumbu za mauaji hayo na watu wote wanaohitaji msaada ndio vimenihamasisha kujiunga na WFP” 

Kwa Liberee sio tu anahisi uchungu wa madhila ya wakimbizi bali pia anaelewa jukumu kubwa la chakula kwa jamii zilizo hatarini zinazokimbia vita. 

Na anasema asilani hatosahau msaada wa chakula waliopewa na WFP wakati huo ambao uliokoa maisha yake na ya maelfu ya Wanyarwanda wengine. Na anaamini kwamba sasa “dunia nzima inaelewa kwamba msaada wa kibinadamu wa chakula ni muhimu sio tu kwenye vita na majanga bali pia katika kushirikiana na serikali zote duniani katika kufikia lengo la kutokomeza njaa.” 

WFP bado inaendelea kutoa mgao wa chakula kwa takriban wakimbizi 138,000 kutoka nchi jirani za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC. 

Audio Credit
UN News/John Kibego
Audio Duration
2'12"
Photo Credit
WFP/Jonathan Eng