Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chanzo cha mizozo lazima kishughulikie kuhakikisha ajenda ya maendeleo inatimia:UN

Chanzo cha mizozo lazima kishughulikie kuhakikisha ajenda ya maendeleo inatimia:UN

Pakua

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema kushughulikia mazingira hatarishi na mzozo ni nguzo muhimu kwa ajili ya amani na usalama huku akisema mambo hayo pia ni kizuizi kikubwa katika kutekeleza ajenda ya mwaka 2030 ya maendeleo endelevu. Grace Kaneiya na taarifa zaidi

(TAARIFA YA GRACE KANEIYA)

Katibu Mkuu amezungumza hayo kwenye kikao cha wazi cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichofanyika leo mjini New York Marekani kwa njia ya mtandao kuhusu changamoto za kuwepo kwa amani na usalama katika mazingira hatarishi,  

Bwana Guterres ameongeza kuwa hata kabla ya janga la corona au COVID-19, hali ya mizozo ilikuwa inazorota na kwamba,“mizozo imekuwa tata zaidi, ikichangiwa na hali za kikanda, kuibuka kwa makundi yaliyojihami na ushirikiano wao, uhalifu na misimamo mikali ambayo inadumu kwa muda mrefu na ni vigumu kuitatua.” 

 Kwa mujibu wa ripoti ya Benki ya Dunia kuhusu maeneo hatarishi na yenye mizozo, mtu mmoja kati ya watano Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini anaishi karibu na mzozo mkubwa na kwa mantiki hiyo mahitaji ya kibinadamu yameongezeka na kufikia viwango vya juu tangu vita ya pili yva dunia. 

Aidha idadi ya watu walio hatarini kufa njaa imeongezeka maradufu na mbinu za kutatua mizozo zimefika ukomo. 

Katibu Mkuu huyo amesema janga la COVID-19 limefanya hali ambayo ilikuwa mbaya kuwa mbaya zaidi na kwamba, “mwaka 2020 kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 22, umasikini uliokithiri uliongezeka na hali hatarishi na mzozo huenda ikatumbukiza watu wengine milioni 18 hadi 27 katika umasikini. Pengo la usawa wa kijnisia linaendelea kupanuka na ushiriki wa wanawake kwenye sekta ya ajira umekuwa ukirudi nyuma kwa miongo kadhaa. Mabadiliko ya tabianchi ni kichocheo cha ukosefu wa usalama na sio sifa kwamba kati ya nchi 15 zilizohatarini kwa athari za mabadiliko ya tabinachi nane zina Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa operesheni za amani au ujumbe mahususi wa kisiasa. "

Bwana Guterres ameongeza kuwa, “iwapo minyororo ya umasikini na mizozo itakatwa hatua mathubuti zinahitajika ikwemo mosi, ushirikiano, Ajenda ya 2030 inatambu kwamba hakuwezi kuwa na maendeleo endelevu bila amani na amani bila maendeleo endelevu kwa hiyo mpango jumuishi wa kujenga amani ya kudumu kwa kuwekeza katika maendeleo ya kibinadamu na amani muhimu.” Pili, “azimio la kutomuacha yeyote nyuma ni lazima liwe katikati ya juhudi zetu kwa ajili ya kuimarisha maendeleo endelevu pamoja na kuzuia na kutatua mizozo.” 

Katibu Mkuu huyo amesema kwamba mzozo na maeneo hatarishi vimekuwa dhahiri hususan barani Afrika akitolea mfano Pembe ya Afrika na ukanda wa Sahel ambapo hali imekuwa mbaya zaidi kwa sababu ya mabadilikoo ya tabianchi, ugaidi, uhalifu wa kupangwa na kuibuka kwa makundi yaliyojihami. 

Katika kukabiliana na hilo Umoja wa Mataifa umefanya kazi kwa karibu na muungano wa Afrika, AU na jamii za kikanda za kiuchumi.  

Bwana Guterres ameongeza kwamba Umoja wa Mataifa umedhamira kuunga mkono ajenda ya AU ya mwaka 2063. 

Katibu Mkuu amekumbusha wito wake wa ufadhili kwa ajili ya kujenga amani kama njia mujarabu ya kukabiliana na mizozo 

Aidha bwana Guterres amekumbusha nafasi muhimu ya Baraza la Usalama katika kushughulikia hali hatarishi na mizozo kwa kuchukua hatua mapema na kuzuia na kutatua mizizi ya mizozo na kuzungumza kwa sauti moja na kwamba, “Baraza linauwezo wa kushawishi jamii ya kimatida kisiasa na kiuchumi na kuangazia maeneo muhimu ya mahitaji na kuhakikisha dhamira ya wadau kwenye mizozo panapohitajika."

Audio Credit
UN News/Grace Kaneiya
Audio Duration
3'41"
Photo Credit
© UNHCR/Sylvain Cherkaoui