Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO Tanzania yawasaidia wakulima kurutubisha lishe kupambana na utapiamlo

FAO Tanzania yawasaidia wakulima kurutubisha lishe kupambana na utapiamlo

Pakua

Nchini Tanzania shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) kwa kushirikiana na serikali na wadau wake wameandaa mpango wa miaka mitano wenye lengo la kuoanisha shughuli za kilimo na lishe ili kukabiliana na utapiamlo. Devota Songorwa wa Radio washirika KidsTime FM ametuandalia taarifa hii kutoka Dodoma nchini Tanzania.

(TAARIFA YA DEVOTHA SONGORWA)

Ni Stella Kimambo, Afisa Lishe wa FAO Tanzania akizungumzia msingi wa mpango huo wa kukabiliana na utapiamlo akisema wamepitia mpango jumuishi wa lishe na mpango wa maendeleo ya kilimo, ASDPII na kuangalia kasoro zilizopo na ndipo wakaandaa mpango wa utekelezaji ili, “Kuhamasisha yale mazao lishe ili mtu ajue kabisa akilima usiuze yote na wewe bakiza ya kula katika familia yako kuweza kuboresha lishe kwa njia ya chakula.”

Bi Kimambo amesema tatizo kubwa ni  “uelewa katika jamii chakula kipi kitumike na kipikwe nako kulikuwa na shida. Halafu uratibu wa mpango jumuishi wa lishe na ASDPII ni sekta zinaratibishwa tofauti. Kwa hiyo tulikuwa tunahitaji kuweka pamoja wadau wanaohusika na afua za lishe zinazohusiana na kilimo tuweze kwenda pamoja tuwe na mpango wa pamoja wa utekelezaji kama ulivyoona wa miaka mitano ili tuweze kuangalia mchango wa chakula katika kupunguza utapiamlo.”

Tulijiuliza kwa nini Tanzania tuna mazao mengi na tunalima vyakula vyenye lishe lakini bado kuna utapiamlo- Stella Kimambo, FAO Tanzania.

Afisa huyo wa FAO amesema mwakani watawaleta pamoja maafisa kilimo na wale wa lishe ili kuwajengea uwezo.

Naye Afisa Kilimo Mkuu Wizara ya Kilimo Margaret Natai akabainisha faida za mpango mpya akisema kuwa, “huko nyuma hatukuwahi kuwa na mpango kama huu. Huu ni mpango wa kwanza ambao tumeuandaa sasa hivi kutekeleza lishe katika kilimo. Huko nyuma tulikuwa tunatekeleza kiholela holela. Kwa hiyo tunajipanga vizuri, na kwa kuwa na huu mpango tutaweza kujiratibu vizuri na tunaweza kufanya ufuatiliaji.”

Sauti
2'12"
Photo Credit
WFP/Hugh Rutherford