Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkazi wa Sudan Kusini: Sioni sababu ya mtoto wa kike kuwa na thamani zaidi kuliko ng'ombe

Mkazi wa Sudan Kusini: Sioni sababu ya mtoto wa kike kuwa na thamani zaidi kuliko ng'ombe

Pakua

Nchini Sudan Kusini, wakazi wa jimboni Bahr-el-Ghazal wameelimishwa jinsi ya kuripoti matukio ya ukatili wa kingono na unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya wanawake, tukio ambalo limechagizwa na ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo. John Kibego na taarifa kamili.

Ndani ya moja ya studio za redio ya jamii jimboni Bahr-el-Ghazal, kaskazini-magharibi mwa Sudan Kusini washiriki wanajadili harakati za kukabili ukatili wa kijinsia. Miongoni mwao ni Maria Angelo mkazi wa Aweil akieleza jukumu lao. 

Maria anasema,  "ni jukumu letu vijana kubaini na kujitambua sisi ni nani, bila kujali tamaduni zetu zinatutumbukiza kwenye nini. Kwa sababu iwapo ukiangalia tamaduni zetu, mtoto wa kike anapaswa kuolewa ili familia ipate ng’ombe. Lakini ng’ombe hapaswi kuwa kipaumbele. Tunahitaji kwenda shule na kusoma ili tubadili jamii zetu na tulete maendeleo.”

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini, UNMISS uliandaa mjadala kupitia radio tatu za kijamii ambapo washiriki walitumia lugha za kienyeji kuvunja ukimya katika masuala ambayo huonekana mwiko kujadili kama vile ndoa za umri mdogo na ubakaji.

Balozi wa vijana, Joseph Adoung amesema mjadala wa aina hiyo ni muhimu na anatumai kuwa jami itachukua hatua kwa kusikiliza na kusaidia kutokomeza ukatili wa kjinsia dhidi ya wanawake na wasichana kuanzia ngazi ya familia hadi taifa.

Rebecca Abour ambaye ni waziri wa zamani wa masuala ya watoto na maendeleo ya jamii nchini Sudan Kusini anasema kuwa dhima ya vyombo vya habari ni kubwa mno katika kutokomeza ukatili wa kjinsia kwa kuwa ujumbe unatafsiriwa kwa lugha za wenyeji.

UNMISS kupitia afisa wake wa masuala ya kijamii, Mariama Dauda inasema kuwa walibaini umuhimu wa vipindi vya radio kufikia hadhira zilizo mbali na ambazo pengine hazina fursa za kupata ujumbe wa aina hiyo.

Mariama anasema, “tumeamua kutumia vipindi vya mijadala vya redio badala ya mikutano na mikusanyiko na imekuwa na matokeo mazuri sana. Zaidi ya yote tulitumia lugha za wenyeji kwa sababu Radio Miraya haiko kila pahali.”
 


 

Audio Credit
Anold Kayanda/John Kibego
Sauti
2'5"
Photo Credit
UNMISS\Nektarios Markogiannis