Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuna njaa, ni maafa, asema mkimbizi wa Syria aliyeko Lebanon. UNHCR inajitahidi kusaidia. 

Tuna njaa, ni maafa, asema mkimbizi wa Syria aliyeko Lebanon. UNHCR inajitahidi kusaidia. 

Pakua

Ripoti hiyo ya Benki ya Dunia na UNHCR imechunguza madhara ya ugonjwa wa COVID-19 katika kuwasukuma wakimbizi wa Syria katika umaskini, wao pamoja na wenyeji wao nchini Jordan, Lebaon na aneo la Kurd nchini Iraq.  Ahimidiwe Olotu na taarifa zaidi.

Ripoti hiyo inasema watu wanaokadiriwa kufikia milioni 4.4 katika jamii wenyeji, na pia takribani wakimbizi milioni moja wa Syria, na Wairaq wengine 180,000 waliokimbia makazi yao wameanguka chini ya mstari wa umaskini tangu mwanzo wa janga la COVID-19. 

Mfano ni Abdel Nasser Mohomad Al Mahmoud ni kijana mdogo mkimbizi kutoka Syria anayeishi Lebanon aliyeanza kufanya kazi akiwa na umri wa miaka 12.  Katika kipindi hiki cha janga, baba yake alipopoteza kazi yake kutokana na hali ya mambo kuharibiwa na COVID-19, Abdel-Nasser amelazimika kuihudumia familia nzima. Amekuwa akikusanya takataka ambazo zinaweza kutumika tena kuunda vitu vingine, lakini kutokana na COVID-19 amelazimika kutafuta kazi ya ziada.  

Abdel-Nasser anasema, “kuna kazi chache, kwa hivyo nimeanza kufanya kazi na wakulima, kupanda ndimu. Kazi zilikuwa chache kabla ya virusi vya corona, na sasa ni chache zaidi.”  

Familia hiyo iliyakimbia makombora mazito huko Syria mnamo 2013. Sasa wanapaswa kushinda vita tofauti.Ayoush Yassin Al Ali ni mama yake Abdul Nasser, anasema, “tuko katika vita tofauti. Hii ni kama vita. Njaa inaua watu. Hali hii ya njaa na kuona watoto wangu na sisi tuna njaa. Ni maafa mazito." 

Familia ya Abdul Nasser wanaishi kwa msaada mdogo wa fedha wanaoupata kutoka UNHCR. Ingawa msaada huo unawaokoa, lakini hautoshi.  Mama yake Abdel, anasema, “UNHCR inatusaidia lakini msaada hutoshi chakula chetu cha wiki moja. Ni siku mbili zimepita tangu nimepika chochote. Tumeishiwa na gesi ya kupikia. Tunateseka sana.” 

Kijana Abdel Nasser Mohomad Al Mahmoud anasema kwa hali ya sasa ya virusi vya corona ilivyo, hakuna kazi ya kufanya, ni vema asaidie wazazi wake kuliko kwenda shuleni. 

Ripoti hiyo ya Benki ya Dunia na UNHCR imeshauri kuwa mpango wa msaada wa fedha taslim unaosaidia kukabiliana na athari, inabidi uongezwe kwa wakimbizi hao, katika mwaka ujao wa 2021. 

Audio Credit
Anold Kayanda/Ahimidiwe Olotu
Sauti
2'36"
Photo Credit
UN News