Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Loise Wairimu-Virusi vya corona vilibadilisha matarajio yangu katika UN lakini nimejifunza SDGs

Loise Wairimu-Virusi vya corona vilibadilisha matarajio yangu katika UN lakini nimejifunza SDGs

Pakua

Janga la ugonjwa wa COVID-19 unaosababishwa na virusi vya Corona limevuruga ndoto za mamilioni ya watu kote duniani. Elimu, afya, biashara, utalii, ukuaji wa kiuchumi na kadhalika vimeyumba kwa kiasi kikubwa. Assumpta Massoi na maelezo zaidi.

Mmoja wa waathirika wa hali hiyo ni msichana Loise Wairimu ambaye mnamo mwezi Machi mwaka huu alisafiri kutoka Nairobi Kenya kuja katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa New York Marekani ambako alitegemea kupata mafunzo kwa vitendo lakini hali haikwenda kama alivyotarajia kwani jengo la Umoja wa Mataifa lilifungwa ikiwa ni moja ya njia ya kupambana na virusi hivi hatari. Loise anasema,  

“Nilipofika nakumbuka nilienda ofisini kwa wiki mbili, halafu ikabidi tuanze kufanyia kazi nyumbani. Kwa hivyo hiyo ilibadilisha akili yangu si kitu ambacho nilikuwa nakitarajia. Lakini katika mwezi Machi nilikuwa nafikiri COVID-19 itaisha na tutarudi ofisini lakini nikaona inazidi kuongezeka kwa hivyo ikabidi nitafute namna ya kufanyia kazi nyumbani, kujifunza na naweza kufurahia wakati wangu hapa.” 

Je, kufanyia kazi nyumbani, kulikuwa na changamoto gani kwake? Loise anaeleza,  

“Kwanza Kabisa ningependa kusema kuwa kufanyia kazi nyumbani ni jambo gumu sana, sana, sana kwa vile hata sijawahi kufanyia kazi nyumbani. Ninajua kwenda ofisini kukaa kwenye kiti kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa kumi jioni. Kwa hivyo kufanya kazi ilikuwa kazi ngumu sana kwa vile inabidi ujiambie uamke, ujiambie ufanye kazi hakuna mtu anakuambia fanya hiki.”  

Mabango ya maendeleo endelevu kama yanavyoonekana katika viwanja vya Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani Septemba 20,2019
UN News/Conor Lennon
Mabango ya maendeleo endelevu kama yanavyoonekana katika viwanja vya Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani Septemba 20,2019

Waswahili wanasema hakuna ziada mbovu, pamoja na changamoto zote hizi, Loise Wairimu amejifunza nini katika Umoja wa Mataifa? Anafafanua, 

“Nimejifunza mambo mengi sana kuhusu SDGs, Malengo ya maendeleo endelevu. Mambo ambayo kabla sijaingia katika Umoja wa Mataifa nilikuwa nikiyasikia kwa umbali, lakini nilipokuja hapa na kufanya taarifa ambazo zinahusiana na mambo ya malengo ya maendeleo endelevu, nimejifunza mambo mengi sana na pia imenisaidia kuona namna ninavyoweza kujiweka vizuri ili niweze kuchangia kwa njia moja ama nyingine.” 

 

 

Audio Credit
Assumpta Massoi/Loise Wairimu
Audio Duration
2'10"
Photo Credit
Video screenshot/Loise Wairimu