Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres: Takwimu ni muhimu katika kukabiliana na changamoto za sasa duniani

Guterres: Takwimu ni muhimu katika kukabiliana na changamoto za sasa duniani

Pakua

Katika kuadhimisha siku ya takwimu duniani leo tarehe 20 mwezi Oktoba,  Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema takwimu ni muhimu sana katika kuunda sera kwa kuzingatia ushahidi sahihi na kwamba

“Takwimu zinazokwenda na wakati, za kutegemewa na za kuaminika, zinatusaidia kuelewa mabadiliko ya dunia tunayoishi na kuchagiza mabadiliko yanayohitajika ili kuhakikisha hatumwachi yeyote nyuma.” 

Guterres amesema janga la corona au COVID-19 linaloighubika dunia hivi sasa limedhihirisha umuhimu wa takwimu katika kuokoa maisha na kujikwamua vyema na ndio maana Umoja wa Mataifa umezindua hivi karibuni mkakati wa takwimu kwa ajili ya kila mtu na kila mahali. Kwa mantiki hiyo amesisitiza kwamba,“Siku hii ni fursa ya kutambua wataalam wa takwimu kote duniani ambao wanafanyakazi kutoa takwimu za kuaminika, kuzingatia kanuni za msingi za takwimu rasmi na kujenga mifumo ya ikolojia ya takwimu yenye mnepo na ugunduzi.” 

Guterres ameisihi dunia kuwekeza na kusaidia jukumu muhimu la takwimu katika kutatua changamoto za zama hizi na ujumbe wake umekuja wakati leo limeanza kongamano la siku tatu la kimataifa la takwimu lililoandaliwa na Umoja wa Mataifa kwa njia ya mtandao na kuwaleta pamoja wataalam wa takwimu zaidi ya 5,000 kutoka nchi zaidi ya 100, likijumuisha pia serikali, sekta binafsi, mashirika ya kimataifa, viongozi wa kisiasa na wachagizaji wa maendeleo endelevu. 

Audio Credit
Assumpta Massoi
Audio Duration
1'2"
Photo Credit
UN News