Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Misaada ya kimkakati ni muhimu ili kukwamua nchi zilizotwama kutokana na COVID-19: Tanzania

Misaada ya kimkakati ni muhimu ili kukwamua nchi zilizotwama kutokana na COVID-19: Tanzania

Pakua

Tanzania imezungumza kwenye mjadala mkuu wa mkutano wa 75 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kuelezea msimamo wake katika masuala mbalimbali ikiwemo ushirikiano wa kimataifa, janga la ugonjwa wa Corona, COVID-19, amani na usalama maziwa makuu na mustakabali wa Umoja wa Mataifa wakati huu ambapo chombo hicho kinatimiza miaka 75 tangu kuanzishwa kwake.

Misimamo hiyo ya Tanzania imetolewa na Rais John Magufuli wa Tanzania kupitia hotuba iliyosomwa kwa niaba yake kwenye ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hii leo na Mwakilishi wa kudumu wa taifa hilo kwenye Umoja huo, Balozi Profesa Kennedy Gastorn.

Kupitia hotuba hiyo Balozi Gastorn amesema , "nina heshima kubwa kuwasilisha hotuba hii kwa niaba ya Rais John Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye hakuweza kuungana nanyi kwa njia ya mtandao kwa kuwa hivi sasa anashiriki kampeni za uchaguzi mkuu zinazoendelea nchini humo. Rais Magufuli anawania awamu ya pili ya uongozi kwenye uchaguzi utakaofanyika tarehe 28 mwezi ujao wa Oktoba.”

Ametumia sehemu ya mwanzo ya hotuba yake kusema kuwa Tanzania imesisitiza azma yake ya kwamba kampeni na uchaguzi vinafanyika kwa amani, huru, uhalali na kwa uwazi kama ambavyo imekuwa ikifanya tangu mwaka 1965.

Akizungumzia janga la Corona au COVID-19, amepigia chepuo ushirikiano wa kimataifa akisema umedhihirisha umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika kukabili changamoto kama janga la Corona ambalo pamoja na kusababisha vifo, limevuruga uchumi wa nchi na dunia nzima.

Amesema ni katika muktadha huo huo, Tanzania inashukuru juhudi zote ndani ya Umoja wa Mataifa za kuhamasisha juhudi za kukabili janga hilo na kwa Tanzania shughuli za kiuchumi na kijamii zimerejea katika hali ya kawaida lakini, “Hatuwezi kukana madhara ya janga hilo kwa nchi yetu na duniani kwa ujumla hasa kwa nchi maskini na zile zinazoendelea, tunashukuru wadau wetu wa maeneleo ikiwemo taasisi za fedha za kimataifa ambazo zimesaidia juhudi zetu za kutokomeza janga hilo kwa kutupatia unafuu kwenye ulipaji madeni, kuahirisha ulipaji madeni na hata kutupatia mikopo yenye riba nafuu na pia msamaha wa madeni ili nchi maskini na zile zinazoendelea ziweze kujikwamua kiuchumi.”

Kuhusu miaka 75 ya Umoja wa Mataifa, Tanzania imesisitiza azma ya pamoja na mataifa mengine ya kuendelea kusimamia na kuzingatia misingi ya Umoja wa Mataifa ambayo ni amani na usalama, haki za binadamu na maendeleo.
Akimulika ushirikiano wa kimataifa, amesema bila shaka ni mbinu muhimu ya kufanikisha ushirikiano baina ya mataifa.

 “Tunapoingia muongo wa utekelezaji kuelekea ukomo wa ajenda 2030 tunaendelea kuamini kuwa Umoja wa Mataifa ni jukwaa pekee la kujadili changamoto za dunia.”

Ametamatisha hotuba yake kwa kusisitiza msimamo wa Tanzania katika kutoa msaada wowote kwa Umoja wa Mataifa ili kufanikisha ajenda ya dunia ikiwemo kusongesha usawa, kujitawala, amani, usalama, haki za binadamu, maendeleo, ajenda 2030 na marekebisho ya Umoja wa Mataifa.
 

Audio Duration
2'59"
Photo Credit
UN Webccast