Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mafuriko Sudan Kusini yaongeza chumvi kwenye kidonda, watu walia njaa.  

Mafuriko Sudan Kusini yaongeza chumvi kwenye kidonda, watu walia njaa.  

Pakua

Shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa WFP linasema hali ya kibinadamu nchini Sudan Kusini inaendelea kuzorota kwa kasi wakati wimbi la njaa likienea katika nchi ambayo ina mgogoro, mvua kubwa na mafuriko ambayo yanavuruga upatikanaji wa chakula kwa watu. Ahimidiwe Olotu amefuatilia taarifa hiyo na haya ni maelezo yake. 

Mvua kubwa zimesababisha mito kujaa maji na hivyo kusababisha mafuriko katika eneo kubwa na makazi ya watu katika maeneo ya White Nile na pia kuua mifugo ambayo ni chanzo kikuu cha maisha ya watu katika jimbo la Jonglei. 

Gari ambalo linaweza kupita katika barabara zilizofunikwa na maji ni gari hili maalumu la WFP ambalo limetengenezwa mahususi kumudu hali mbalimbali.

Kwa upande wa wananchi, njia iliyobaki ni kukanyaga kati maji au kupanda mtumbwi. Zaidi ya watu 700,000 kote Sudan Kusini wameathiriwa na mafuriko tangu mwezi Juni na WFP imetoa msaada kwa watu wapatao 500,000 hadi kufikia mwezi Agosti.

Adol Kur Akuei, mama wa watoto 7 ambaye amefurushwa na mafuriko na sasa anaishi Bor, kwa lugha ya Dinka anasema, “katika Kijiji nilikotoka, kinachoitwa Mathiang, mafuriko yalikuwa makubwa. Yaliharibu kila kitu. Yaliharibu nyumba zetu, yakaua ng’ombe wetu, mazao yetu na kila chanzo cha maisha. Tumekuwa hapa kwa takribani mwezi mmoja na hatujapokea msaada wowote. Tunakufa kwa njaa. Tunahitaji chakula.”  

Mkurugenzi wa WFP Sudan Kusini Matthew Hollingworth anasema WFP itabidi kuwasaidia takribani watu 600,000 katika msimu huu na akaongeza, “tunafahamu kuwa tuna vifaa kwa ajili ya kazi hii na tuna watu na wadau katika eneo. Lakini tuna uhitaji mkubwa wa dola milioni 58 za kimarekani ili kutoa msaada wa haraka kwa jamii lakini pia muhimu zaidi kuwawezesha kusimama punde tu watapoweza kurejea nyumbani.”  

WFP inasema janga la COVID-19 linaendelea  kudhoofisha hali ya kibinadamu ambayo tayaroi ilikuwa tete lakini shirika hilo linajitahidi kuongeza msaada wake ili kuyafikia mahitaji ambayo yanaongezeka.  

Audio Credit
Flora Nducha/Ahimidiwe Olotu
Sauti
2'7"
Photo Credit
© WFP/Musa Mahadi