Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tanzania tuna imani na UN, lakini ijitathmini nasi wanachama tujitathmini

Tanzania tuna imani na UN, lakini ijitathmini nasi wanachama tujitathmini

Pakua

Mjadala Mkuu wa mkutano wa 75 wa Baraza Kuu  la Umoja wa Mataifa, UNGA75 unafunga pazia leo Jumanne ambapo miongoni mwa nchi za Afrika zitakazohutubia ni Tanzania, ambayo imesema ujumbe wake mkuu kwenye jukwaa hilo ni kueleza kuwa bado ina imani kubwa na chombo hicho chenye wanachama 193. Flora Nducha na maelezo zaidi.

Akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, UN News Kiswahili, Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa Profesa Kennedy Gastorn, ambaye ndiye atasoma hotuba hiyo kwa niaba ya Rais John Magufuli amesema,“ujumbe mkubwa kwanza ni huu, sisi tuna imani kubwa sana na Umoja wa Mataifa kama chombo ambacho kinaweza kuratibu shughuli za nchi zote duniani, kama chombo muhimu ambacho kwa kweli ni kama Bunge la dunia tunapokwenda kwenye Baraza Kuu. Hilo ni moja! "

Hata hivyo amesema ni muhimu pia kusititiza, “Umoja wa Mataifa ujitathmini, na sisi pia kama wanachama wa Umoja wa Mataifa lazima tujitathmini katika ngazi ya nchi na katika ngazi ya umoja wetu. Tukishajitathmini basi tuweze kuwa na uhalisia katika kusaidia  ili kuweza kusaidia kutekeleza majukumu yake kama ilivyoanishwa kwenye chata yake.”

Sajini Tekla Kibiriti wa kikundi cha 7 cha kikosi cha TANZBATT 7 kilichoko kikosi cha kujibu mashambulizi cha MONUSCO, FIB, akitoa huduma ya afya kwa wanawake wakazi wa kata ya Matembo iliyoko Beni jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya
TANZBATT 7/Ibrahim Mayambua
Sajini Tekla Kibiriti wa kikundi cha 7 cha kikosi cha TANZBATT 7 kilichoko kikosi cha kujibu mashambulizi cha MONUSCO, FIB, akitoa huduma ya afya kwa wanawake wakazi wa kata ya Matembo iliyoko Beni jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

 

Akazugumzia pia hoja ya Afrika kuhusu Umoja wa Mataifa akisema, “tunakwenda na ujumbe kwamba kama Afrika tuna mapendekezo ya maboresho ambayo tungependa sana Umoja wa Mataifa tuweze kuipa nafasi Afrika katika kuboresha mifumo ya utawala ndani ya Umoja wa Mataifa. Lakini pia ni wakati mwingine ambapo sisi kama nchi ni muhimu pia kutoa mchango katika baadhi ya mambo makubwa sana ya kimataifa yanayoendelea hapa duniani ambayo tuna michango mingi katika na maslahi yetu, na kama nilivyosema ni chombo ambacho kila nchi kinapaswa kulinda maslahi yake.”

Katika mjadala huu mkuu ulioanza tarehe 22 mwezi huu wa Septemba, wakuu wa nchi na serikali pamoja na mawaziri wametoa hotuba zao kwa njia ya mtandao kutokana na vikwazo vya janga la Corona au COVID-19 ambavyo vimelazimu mkutano kufanyika kwa mtandao na kutoka ukumbini.

Hata hivyo ukumbini waliopo ni wawakilishi wa kudumu wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa na kwamba hata Balozi Gastorn atahutubia kutoka ndani ya ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

 

Audio Credit
Flora Nducha/Balozi Kennedy Gastorn
Audio Duration
2'18"
Photo Credit
UN News/Anold Kayanda