Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Katika kutunza mazingira, UN huiona Tanzania kuwa ni nchi ya kimkakati.

Katika kutunza mazingira, UN huiona Tanzania kuwa ni nchi ya kimkakati.

Pakua

Kuelekea mkutano wa viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuhusu bayonuai tarehe 30 mwezi huu wa Septemba, Tanzania imezungumzia ujumbe wake kwenye mkutano huo wakati huu ambapo baadhi ya mataifa hayaamini umuhimu wa bayonuai katika mustakabali wa binadamu na mazingira.

Akizungumza na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Kennedy Gastorn amesema ujumbe wao ni dhahiri kwa kuzingatia kuwa tayari Tanzania ina mkakati wa kitaifa wa bayonuai kwa hiyo kwenye mkutano huo, “ujumbe wetu mkubwa sana kwanza ni kuweza kuhimiza ujumbe wa bayonuai ili hata wale ambao hawaamini waweze kuamini. Lakini tutawasisitiza kwamba hili ni jambo linalohitaji ushirikiano wa kimataifa, nchi moja hata ikitunza haiwezi kusaidia sana. Kwa hiyo sisi tutawaonesha tulichofanya na kuwaeleza umuhimu wake."

Amekumbusha kuwa suala la uoto wa asili akisema kuwa, "hasa ule uoto wa asili, yale mapori tengefu, misitu ambayo tumehifadhi, hayo ndio mambo tunataka tuwaoneshe kwamba siyo tu mambo ya kuandika kwenye sera na sheria zetu, lakini pia wakifika pale wataweza kuona uhalisia. Zaidi ya asilimia 30 ya nchi ya Tanzania ni maeneo ya uhifadhi na huko ndiko ambako bayonuai iko na ndiko uhifadhi wetu upo.

Utunzaji na utumiaji endelevu unaweza kufanya kazi pamoja kulinda mimea na wanyama wanaoishi katika misitu.
©UNEP/Jessica Kerr
Utunzaji na utumiaji endelevu unaweza kufanya kazi pamoja kulinda mimea na wanyama wanaoishi katika misitu.

Balozi Gastorn akaelezea ni kwa vipi Tanzania inatazamwa na Umoja wa Mataifa kama nchi ya kimkakati katika kutunza mazingira kwa kuwa, "katika mkakati wa dunia wa kupambana na mabadiliko ya tabianchi, kitu kikubwa sana ni mapori ya asili. Mapori ya asili yana uwezo mkubwa sana wa kuleta mabadiliko kuliko mapori au miti ya kuipanda. Hata hivyo tunaendelea kuilinda misitu ya asili na tunaendelea kupanda misitu ya kawaida. Na ndio maana nchi zote zenye miti mingi au mapori ya asili kama Tanzania zinakuwa ni nchi za kimkakati na Umoja wa Mataifa unaziangalia hizo nchi kwa jicho la kipekee kabisa. Kwamba ni muhimu kwanza zikawezeshwa kutokuharibu maeneo hayo waliyonayo, lakini pia kuweza kujifunza ni namna gani hata nchi ambazo zimepoteza maeneo ya asili zinaweza labda kujifunza zikaweza kuyarejesha.”
 

Bayonuai ni utofauti wa uhai katika dunia ambao hupimwa kwa kuangalia uwepo wa pamoja wa aina mbali mbali za mimea, wanyama na wadudu na mfumo wa kiekolojia.

Audio Credit
Flora Nducha/Balozi Kennedy Gastorn
Audio Duration
2'17"
Photo Credit
FAO/Giulio Napolitano