Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kunenepesha na kuuza kondoo ni biashara inayoinua kipato cha familia Sahel

Kunenepesha na kuuza kondoo ni biashara inayoinua kipato cha familia Sahel

Pakua

Katika ukanda wa Sahel, ufugaji ndio chanzo kikuu cha kipato kwa zaidi ya wakazi milioni 20 wa eneo hilo ambao hata hivyo leo hii asilimia 40 ya watu hao wako kwenye lindi la umaskini na waliosalia wako hatarini kutumbukia kwenye umaskini. Ahimidiwe Olotu anaeleza zaidi. 

Ni katika kuepusha hali hiyo Benki ya Dunia imeanzisha mradi uliowawezesha wakazi zaidi ya 20,700 kwenye ukanda wa Sahel kupata mafunzo, vifaa na mtaji wa kupanua mradi wa ufugaji ili uwe wa kisasa zaidi na hivyo kuongeza kipato cha familia.

Miongoni mwao ni Adiara Sanogo, mkazi wa Sikassa nchini Mali ambaye anasema, “mwanzoni watu hawakuamini kuwa mwanamke anaweza kufuga mifugo na kuinenepesha kwa ajili ya kuuza. Lakini leo hii kila mtu anajivunia maendeleo yangu. Kwa hiyo nimepanga kuendeleza mradi huu, na punde nitaweza kukimu mahitaji ya familia yangu.”

Adiara alipata mtaji na mafunzo kutoka Benki ya Dunia na alichofanya alinunua kondoo, akawanenepesha na kisha kuwauza. Fedha aliyopata ilimwezesha kununua ng’ombe na kiasi kilichobakia alihifadhi kwa ajili ya kununulia vifaa vya shule vya watoto wake.

“Ninaamini  kuwekeza kwenye ng’ombe kutaniletea faida zaidi. Na baada ya kumuuza huyu ng’ombe nitanunua kondoo wengine na nianze tena," anasema Adiara.

Kuweka akiba

Mafunzo waliyopata kutoka Benki ya Dunia yalihusisha pia kuwa makini katika matumizi ya fedha ili hatimaye waweze kujitegemea na hivyo Adiarra anasema “hivi sasa sili faida.”

Mradi huo wa ukanda wa Sahel wa kusaidia wafugaji, PRAPS umelenga zaidi ya wakulima wafugaji milioni 2. 

 

Audio Credit
Flora Nducha/Ahimidiwe Olotu
Audio Duration
1'37"
Photo Credit
Photo: FAO/Marco Longari