Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN: Mjadala wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa UNGA75 wafungua pazia

UN: Mjadala wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa UNGA75 wafungua pazia

Pakua

Mjadala wa Mkuu wa ngazi ya juu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa UNGA75 leo umefungua pazia rasmi kwenye makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani na mtandaoni ukiwaleta pamoja nchi zote wanachama wa Umoja huo 193.  Flora Nducha na maelezo zaidi.

Akifungua mjadala huo Rais wa Baraza Kuu Volkan Bozkir amesema  

“nawaomba nchi zote wanachama kutoa ushirikiano na mshikamano kwa chombo hiki na kuwa wabunifu ili kuhakikisha kinaendelea kutimiza wajibu wake na kuwa na umuhimu  sasa na kwa vizazi vijavyo. Na kuhakikisha hakuna anayesalia nyumba lazima kuongeza juhudi katika kila lengo la SDGs na kukabili kwa pamoja janga la COVID-19 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres hotuba yake imejikita katika mambo makuu matano, janga la COVID-19, vita na athari zake za kibinadamu, malengo ya maendeleo endelevu SDGs, miaka 75 ya Umoja wa Mataifa na changamoto inayotishia mustakbali wa duinia ya mabadiliko ya tabianchi.  

Amesema changoto kubwa za dunia hii haziwezi kutatuliwa na mtu mmoja bali kwa mshikamano wa kimataifa kwani,“kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 30 umasikini unaongezeka, viashiria vya maendeleo ya binadamu vinashuka, tunakwenda kombo katika ufikiaji wa malengo ya maendeleo endelevu. Wakati huohuo juhudi za kukomesha utengenezaji wa silaha za nyuklia zinakwenda mrama na tunashindwa kuchukua hatua katika maeneo kunakoibuka hatari hususan kwenye mitandao. Watu wanaumia, sayari yetu inateketea, dunia yetu inahaha, ina shinikizo na inasaka uongozi wa kweli na hatua.”  

Katika janga la corona amesema hakuna aliye salama hadi kila mtu atakapokuwa salama, ametoa mapendekezo haya kwa nchi wanachama, "kuzikabili changamoto hiizi tunahitaji ushirikiano zaidi wa kimataifa na si upungufu, tunahitaji kuimarisha taasisi za mikataifa na sio kkujitenga nazo, na tunahitaji uongozi bora wa kimataifa na sio vurugu kwa kila mtu." 

Kama ada ya kila mwaka katika mjadala wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa Brazil huzungumza ya kwanza na leo akihutubia mjadala huo kwa njia ya video Rais wa Brazil Jair Bolsonaro, amemulika janga la COVID-19 akisema kuwa “mwanzoni kabisa nilionya kuwa tuna matatizo mawili ya kutatua; COVID-19 na ukosefu wa ajira na kwamba matatizo yote hayo mawili yanapaswa kushughulikiwa pamoja kwa kiwango sawia cha uwajibikaji. Hatua zote za kutochangamana zilizizngatiwa katika majimbo yote 27.” Amerushia lawama vyombo vya habari kwa kile alichodai kuwa vilijenga hofu kwa wananchi lakini serikali yake ilisimama kidete na kuhakikisha rasilimali zinazohitajika na misaada inafikia wananchi. 

Rais wa Marekani Donald Trump akiwa wa pili kuzungumza katika mjadala wa ngazi ya juu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa UNGA75, ameeleza namna Marekani ilivyofanya jitihada za kuudhibiti ugonjwa wa COVID-19 akisema kuwa kwa haraka walisambaza vifaa vya kusaidia kupumua, na pia wakatengeneza vya ziada kiasi cha kusambaza kwa marafiki na wadau wao kote duniani. 

Kuhusu chanjo dhidi ya virusi vya corona Trump amesema, “shukrani kwa juhudi zetu, chanjo tatu ziko katika hatua za mwisho za majaribio. Tunazizalisha nyingi kusudi zisambazwe zitakapowasili. Tutasambaza chanjo, tutavishinda virusi, tutamaliza janga na tutaingia katika enzi mpya ya mafanikio, ushirikiano na amani isiyokuwa ya kawaida.”

 

Nchi zote wanachama zinatarajiwa kuzungumza katika mjadala huo utakaotoa kipaumbele pia katika masuala ya bayoanuwai, miaka 25 baada ya jukwaa la Beijing la kuchukua hatua kuhusu haki za wanawake na mustakbali wao, maadhimisho ya miaka 75, ufadhili wa fedha katika kujikwamua na janga la COVID-19 na malengo ya maendeleo SDGs ikiwa imesalia miaka 10 tu kabla hayajifikia ukomo hapo 2030. 

Audio Credit
Flora Nducha
Audio Duration
2'14"
Photo Credit
UN Photo/Cia Pak