Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miaka 10 baadaye, hatimaye misaada ya UN yawafikia katika milima ya Jebel Marra, Sudan. 

Miaka 10 baadaye, hatimaye misaada ya UN yawafikia katika milima ya Jebel Marra, Sudan. 

Pakua

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, limepeleka misaada katika eneo la Jebel Marra, Darfur, Sudan ili kuokoa maisha ya watu waliokimbilia katika maeneo hayo ya milima kuyakimbia mapigano katika maeneo yao. Ahimidiwe Olotu na maelezo zaidi. 

Ngamia waliobeba misaada mbalimbali kutoka shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, wanakatiza polepole katika mabonde na vilima vya mawe.   

Antony Spalton ni Mkuu wa ofisi ya UNICEF ya eneo la Nyala yuko kwenye msafara huo anasema, “tunatembea kuelekea Gorlanbang Jebel Marra ili kufanya tathmini lakini pia kupeleka vifaa vya muhimu kwa ajili ya shule na kliniki.”  

Hii ni mara ya kwanza katika miaka 10, watoa misaada ya kibinadamu kuzifikia jamii hizo zilizotawanywa na mgogoro Kusini mwa Jebel Marra, Darfur, Sudan.  Jebel Marra inapatikana mita 3000 juu ya usawa wa bahari. Njia pekee ya kufika huko ni hii ya kutumia punda au ngamia.  

UNICEF na wadau wake, wamebeba dawa na mahitaji mengine ya kuokoa maisha vikiwemo vifaa vya kupima usalama wa maji na pia dawa ya kutibu maji yaani.   

Msafara umewasili. Watoto na familia zao hapa wanakabiliwa na changamoto. Watoto wengi hawahitimu elimu ya msingi. Asilimia 40 ya watoto wanaostahili kuwa shule hawako shuleni.  

Mtoto mmoja, mdogo wa kike, kupitia mkalimani anaeleza kuwa anaitwa Nassim na kwamba hana vitabu na kuwa darasani wanakaa kwenye mawe.  

El Siddig Musa Abbaker ni Afisa Ufuatiliaji wa  Programu ya UNICEF katika eneo la Kyala, akionesha shule iliyoko nyuma yake ikiwa katika hali mbaya ya magofu anasema, “shule ya namna hii kwa hakika inahitaji pia ukarabati. Kama tunavyoona, kuna vijiji katika maeneo ya karibu na watoto wengi watafaidika na shule hii.” 

Ingawa katika maeneo haya mazao yanakua kwa urahisi kwasababu ya uwepo wa udongo wa volcano, kutokana na ukosefu wa huduma za afya, watoto bado wanakabiliwa na magonjwa yanayozuilika lakini yanayotishia maisha yao kama vile minyoo, kuhara na hata utapiamlo.  

Tatizo jingine hapa ni kuwa watoto wanakatishiwa utoto wao katika umri mdogo kutokana na viwango vya juu vya ndoa za utotoni. Darassalam Mohamed ni Afisa wa kitengo cha ulinzi wa watoto cha UNICEF Nyala anasema,“wakati wa mazungumzo yangu na wanawake na viongozi wa jamii, ninagundua kuwa kuna idadi kadhaa ya ndoa za watoto katika eneo hili. Na ninafikiri tunachopaswa kufanya katika jamii ni kuachana na tabia hiyo.” 

Hii ni safari ya kwanza kati ya kadhaa zijazo kuja hapa Jebel Marra Kusini. Katika miezi ijayo, UNICEF itarejea kusaidia kuwafundisha wanawake na walimu kuhusu kulinda watoto, usafi na elimu na pia kuwapatia misaada ya afya na lishe pamoja na vifaa vya elimu.  

 

 

Audio Credit
Flora Nducha/Ahimidiwe Olotu
Audio Duration
2'51"
Photo Credit
OCHA/Amy Martin