Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miaka 75 tumepiga hatua kubwa na tuna ya kujivunia, lakini safari bado ni ndefu:Guterres

Miaka 75 tumepiga hatua kubwa na tuna ya kujivunia, lakini safari bado ni ndefu:Guterres

Pakua

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema Umoja wa Mataifa una mengi ya kujivunia baada ya kupiga hatua kubwa tangu kuanzishwa kwake miaka 75 iliyopita, lakini bado safari ni ndefu inayohitaji mshikamano wa kimataifa na utashi wa hali ya juu wa kisiasa kukabili changamoto zinazokikikumba kizazi hiki na vijavyo.Jason Nyakundi na maelezo zaidi.

Guterres ameyasema hayo leo kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York katika maadhimisho ya miaka 75 ya Umoja huo yaliyofanyika kwenye kikao cha ngazi ya juu cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa njia ya mtandao. 

Amesema malengo ya Umoja wa Mataifa ambayo ni amani, haki, usawa na utu ndio uti wa mgongo wa mustakabali bora wa dunia lakini miaka 75 inayoadhimishwa leo iliibuka baada ya milima na mabonde. 

Ilichukua vita kuu mbili za dunia, vifo vya mamilioni ya watu na maangamizi makubwa ya mauaji ya Holocust kwa viongozi wa dunia kuweza kutekeleza ushirikiano wa kimataifa na utawala wa sheria na ahadi hiyo ilizaa matunda kwani, “vita ya tatu ya dunia ambayo wengi waliihofia imeweza kuepukwa,haijawahi kutokea katika historia ya hivi karibuni kupita miaka mingi kiasi hicho bila mivutano ya kijeshi baina ya mataifa makubwa yenye nguvu. Haya ni mafanikio makubwa ambayo nchi wanachama wanaweza kujivunia na sote tunapaswa kufanya kila njia kuyalinda.” 

Serikali ya India inahakikisha kwamba vijana wanaojitolea ni sehemu ya mazungumzo na hatua katika kutimiza malengo ya maendeleo endelevu SDGs
© UNDP India
Serikali ya India inahakikisha kwamba vijana wanaojitolea ni sehemu ya mazungumzo na hatua katika kutimiza malengo ya maendeleo endelevu SDGs

 

Mafanikio mengine yaliyopatikana 

Katibu Mkuu amesema katika miongo hiyo zaidi ya saba kumekuwepo na mafanikio mengine mengi mbali ya vita ambayo ni ya kihistoria yakijumuisha mikataba ya amani na ulinzi wa amani, kuweka viwango vya haki za binadamu na mikakati ya kuitekeleza, kutokomeza ubaguzi wa rangi, misaada ya kibinadamu kwa mamilioni ya watu walioathirika na vita na majanga, kutokomeza magonjwa, kupunguza njaa, kupiga hatua katika kuendeleza sheria za kimataifa, mikataba ya kihistoria ya kulinda mazingira na sayari dunia, makubaliano ya malengo ya maendeleo endelevu SDGs, na mkataba wa Paris kuhusu mabadiliko ya tabianchi. 

Hata hivyo amesema pamoja na mafanikio yote hayo “bado kuna kibarua kikubwa cha kufanya. Kati ya wajumbe 850 kwenye mkutano wa san Franscisco wanawake walikuwa wanane tu. Miaka 25 tangu jukwaa la Beijing la kuchukua hatua usawa wa kijinsia unasalia kuwa changamoto moja kubwa zaidi katika suala la haki za binadamu kote duniani. Zahma ya mabadiliko ya tabianchi nayo inanukia, bayoanuwai yetu inatoweka, umasikini unaongezeka, chuki inashamiri, mivutano ya kijiografia inaongezeka na sialha za nyuklia bado ni tishio linalosisimua nywele zetu.” 

Janga la COVID-19 

Katika hotuba yake bwana Guterres pia amesema, pamoja na kwamba teknolojia zimefungua milango ya fursa kubwa lakini pia zimeiweka dunia katika vitisho vipya. 

Mathalani amesema janga la corona au COVID-19 limeweka bayana hali tete inayoikabili dunia na kusisitiza kwamba janga hilo linaweza tu kushughulikiwa kwa pamoja kwani leo hii kuna changamoto lukuki za ushirikiano wa kimataifa ambazo zinakosa suluhu za ushirikiano huo wa kimataifa. 

Akizungumzia la kufanya ili kuganga yajayo Katibu Mkuu amesema huu utakuwa mchakato muhimu na jumuishi kwani tayari dunia inafanhafu tunahitaji kufanya zaidi, kwa ufanisi, ushirikiano wa kimataifa, kwa mtazamo na kuleta mabadiliko. 

“Hakuna anayetaka serikali ya dunia, lakini ni lazima tushirikiane kuboresha utawala wa dunia. Katika dunia hii iliyoungana tunahitaji mtandao wa ushirikiano unaofanyakazi, ambao familia ya Umoja wa Mataifa taasisi za fedha za kimataifa, mashirika ya kikanda, makundi ya biashara na wengine wanafanyakazi kwa pamoja kwa ukaribu zaidi na kwa ufanisi. Pia tunahitaji ushirikiano wa kimataifa ulio jumuishi, unaokumbatia asasi za kiraia, miji, biashara, mamlaka za mashinani na vijana.” 

Mjadala wa kimataifa  

Katibu Mkuu amesema madhimisho haya ya 75 ya Umoja wa Mataifa yanaenda sanjari na mazungumzo ya kimataifa ambayo yaliwafikia watu zaidi ya milioni moja kote duniani yakiwa na mtazamo maalum kwa suti za vijana. 

Katika mazungumzo yao amesema vijana wameeleza hofu na matumaini ya mustakabali wao na kusisitiza kwamba ushirikiano wa kimataifa ni muhimu katika kupambana na changamoto za sasa. 

“Wameeleza kwamba COVID-19 imefanya ushirikiano huo kuhitajika haraka zaidi na wamesisitiza kwamba dunia inahitaji mifumo ya afya na huduma za msingi kwa wote. Watu wanahofu kuhusu mabadiliko ya tabianchi , umasikini, pengo la usawa, ufisadi na ubaguzi wa rangi na wa kijinsia. Wanauona Umoja wa Mataifa kama chombo cha kuifanya dunia kuwa mahali bora. Na wanatutegemea kushinda majaribu haya ya leo, na wajibu huo unaangukia kwa nchi wanachama.” 

Wajibu wa nchi wanachama 

Bwana Guterres amekumbusha kwamba nchi wanachama waliunda Umoja wa Mataifa na wana wajibu wa kuukumbatia, kuuboresha na kuupa nyenzo za kuweza kuleta mabadiliko. 

Tuna deni hilo kwa sisi watu, tuna deni hilo kwa walinda amani, wanadiplomasia, wahudumu wa kibinadamu, na wengine ambao wanajitolewa maisha yao kwa ajili ya kusongesha thamani ya pamoja. Nawaenzi wafanyakazi wote wa zamani na wa sasa kwa kujitoa kwao kwa kuhuisha dhamira za Umoja wa Mataifa.”  

Amesema waasisi wa umoja wa Mataifa walianza kazi yao wakati wa moto wa vita lakini sasa “inatuangukia kusaka njia ya kutoka katika hatari, kama inavyosema katiba yetu hebu tuunganishe juhudi zetu kutimiza malengo haya kama Umoja wa Mataifa.” 

Audio Credit
Flora Nducha/Jason Nyakundi
Audio Duration
3'8"
Photo Credit
UN Photo/Manuel Elías