Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Usalama wa wahudumu wa afya ni msingi wa usalama wa wagonjwa 

Usalama wa wahudumu wa afya ni msingi wa usalama wa wagonjwa 

Pakua

Ikiwa leo ni siku ya usalama wa wagonjwa duniani, shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO limesema hakuna taifa linaweza kuwaweka salama wagonjwa wake iwapo linapuuza usalama wa wahudumu wa afya hasa wakati huu wa janga la ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19 ambalo bado linatikisa maeneo mengi duniani. John Kibego na taarifa kamili. 

Kutana na Souleymane Hamani Zada, mhudumu wa afya katika kituo cha afya cha Guidan Roumdji nchini Niger. Katika zama hizo za COVID-19 anahakikisha amevalia mavazi mahsusi kujikinga yeye na wale anaowahudumia. 

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus amesema kuwa COVID-19 inakumbusha kila mtu juu ya jukumu la wahudumu wa afya katika kupunguza machungu ya wagonjwa na kuokoa maisha, lakini hakuna taifa lolote ambalo linaweza kuwaweka wagonjwa wake salama iwapo litapuuza usalama wa wahudumu wa afya. 

Ni kwa mantiki hiyo, hii leo WHO imezindua katiba ya usalama wa wahudumu wa afya ambayo inaelezea mazingira salama ya kufanyia kazi wahudumu hao, mafunzo wanayohitaji, ujira sambamba na hadhi yao. 

Katiba hiyo inataka serikali na wale wote wanaoendesha huduma za afya kuchukua hatua tano kulinda wahudumu wa afya. 

Hatua hizo ni pamoja na kulinda wahudumu wa afya dhidi ya ghasia, kuimarisha afya yao ya akili, kuwalinda dhidi ya hatari za kimwili na kibailojia, kusongesha miradi ya kitaifa kuhusu usalama wao kazini na kuoanisha sera za usalama wa wahudumu wa afya na zile za usalama wa wagonjwa. 

 Msingi wa katiba hiyo kwa mujibu wa WHO ni kwamba  COVID-19 imewaweka hatarini wahudumu wa afya na familia zao kwenye hatari kubwa, ijapokuwa hakuna takwimu kutoka nchi kadhaa katika kanda zote za WHO ambazo zinadokeza kuwa maambukizi ya COVID-19 miongoni mwa wahudumu wa afya ni makubwa kuliko miongoni mwa jamii. 

 Hata hivyo maelfu ya wahudumu wa afya ambao waliambukizwa virusi vya Corona katika maeneo mbalimbali duniani walifariki dunia. 

Sambamba na katiba hiyo ya usalama wa wahudumu wa afya, WHO imeweka bayana malengo ya afya ya wagonjwa mwaka 2020 ili serikali ziweze kuwekeza, kupima na kuboresha afya ya wahudumu wa afya ifikapo mwakani. 

Kupitia malengo hayo, vituo vya kutoa huduma za afya vinatakiwa kushughulikia maeneo matano: Mosi kuzuia majeruhi, kupunguza msongo utokanao na kazi kupita kiasi, kuimarisha matumizi ya vifaa vya kujikinga na maambukizi, kutovumilia ukatili wowote dhidi ya wahudumu wa afya na kuchambua kwa kina matukio yoyote yanayohusu usalama wa wahudumu hao. 

Audio Credit
Flora Nducha/John Kibego
Audio Duration
2'29"
Photo Credit
UNSOM