Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bado wengine wakihaha kusubiri kufungua shule, UN yatoa mwongozo wa hatua za kufuata

Bado wengine wakihaha kusubiri kufungua shule, UN yatoa mwongozo wa hatua za kufuata

Pakua

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yametoa mwongozo wenye mapendekezo ya mikakati ya kiafya ya kuzingatiwa na serikali kuhusu linin a jinsi ya kufungua tena shule kwenye maeneo ambako shule bado zimefungwa kutokana na janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19. Anold Kayanda na maelezo zaidi.

Mashirika hayo ni lile la elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO, lile la kuhudumia watoto, UNICEF na lile la afya, WHO.
Mapendekezo ni pamoja na ushauri kwa watunga sera ambapo Mkuu wa masuala ya elimu, UNICEF Robert Jenkins amesema, “jamii zinapoanza kufunguka tena baada ya kufungwa kutokana na COVID-19, lazima tuhakikishe kuwa zinapatia kipaumbele cha elimu kwa watoto wetu. Pindi shule zinapokuwa zimefungwa watoto wanakuwa wametengwa, wananyimwa haki zao za msingi za kujifunza, afya na lishe na wanakuwa wako hatarini.”

Bwana Jenkis amesema watoto hao wengi wao wanajikuta wakikumbwa na msongo wakati wakihaha kuendelea na masomo yao nyumbani bila teknolojia inayotakiwa au mbinu za kuwawezesha kufanya hivyo.

“Tuna mifano mingi ya nchi ambazo zinatumia kanuni zetu zilizomo kwenye mwongozo huu ili watoto warejee shuleni na kujifunza, kwa hiyo tunafahamu kile kinachowezekana,”  amesema Jenkins.

Huko nchini Jordan kwenye kambi ya wakimbizi wa kipalestina, shule zimefunguliwa tarehe 1 mwezi Septemba 2020.
UNRWA/Yazan Fares
Huko nchini Jordan kwenye kambi ya wakimbizi wa kipalestina, shule zimefunguliwa tarehe 1 mwezi Septemba 2020.

Mwongozo una mambo yapi?

Mwongozo huo wa kurasa 10 unalenga shule za watoto wenye umri wa chini  ya miaka 18 na unaanza kwa kumulika hali ya maambukizi ya COVID-19, ambapo kuna hatua za kuchukua iwapo hakuna kabisa ugonjwa, au COVID-19 maambukizi ni ya hapa na pale, au kuna eneo maalum au kiwango cha maambukizi ni jamii nzima.

Mathalani iwapo hakuna maambukizi kabisa, bado mwongozo unapendekeza iwapo shule zinafunguliwa, lazima hatua zichukuliwe kuepusha maambukizi ya COVID-19 ikiwemo maeneo ya kunawa mikono kwa maji na sabuni, kuepusha kuchangamana na kuvaa barakoa.

Iwapo maambukizi ni ngazi ya jamii nzima, basi shule zifungwe kwenye maeneo husika na ambako shule hazitafungwa basi kanuni za kuepusha maambukizi zizingatiwe.

Vipi wakati wa kucheza shuleni?

Mashirika hayo yanasema wakati wa michezo shuleni, umbali wa mita moja unapendekezwa na shule zihakikishe kuwa hakuna kuchangamana baina ya madarasa wakati wa michezo, na watoto waelimishwe juu ya umuhimmu wa kutokuwa katika makundi makubwa au kuwepo na umbali wanapokuwa wamepanga mistari au wanapokuwa wanarejea nyumbani.
Halikadhalika wanapendekeza iwapo kuna uwezekano wa kupata walimu wa kujitolea ili kuongeza idadi ya walimu, na madarasa kufanyika asubuhi na mchana ili kupunguza msongamano.

Mawasiliano baina ya wazazi na walimu

Suala la mawasiliano limepatiwa kipaumbele na mwongozo huo unataka kuwepo kwa uwazi katika kutoa taarifa pindi kunapotokea dalili za mtoto yoyote kuugua iwe nyumbani au shuleni.

“Arifu wazazi kuhusu mikakati iliyoko shuleni ya kudhibiti kuenea kwa COVID-19, na omba ushirikiano katika kuripoti kisa chochote cha COVID-19 ambacho kimetokea nyumbani,” unasema mwongozo huo ukiongeza kuwa iwapo kuna mtu nyumbani anashukiwa kuw ana COVID-19, watoto wote kwenye kaya hiyo wanapaswa kubakia nyumbani na shule ipatiwe taarifa.

Ni wapi shule zimefunguliwa hivi sasa?

Kwa mujibu wa ramani ya UNESCO inayoonesha hali ya sasa ya kufunguliwa shule, hadi tarehe 14 mwezi huu wa Septemba nchi ambazo zimefungua tena shule na wanafunzi wamerejea ni Tanzania, Botswana, Afrika Kusini, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Mauritania, Guinea, Chad, China na Urusi.

Kwingineko kama Kenya na Uganda, shule bado zimefungwa na maeneo kama Marekani na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, baadhi ya watoto wanasoma kwa mtandao na baadhi wanakwenda darasani.

 

Audio Credit
Flora Nducha/Anold Kayanda
Sauti
2'17"
Photo Credit
UNICEF/Habib Kanobana