Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres: Demokrasia ni chachu ya kila kitu katika jamii.

Guterres: Demokrasia ni chachu ya kila kitu katika jamii.

Pakua

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya demokrasia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema demokrasia ni muhimu katika kuhakikisha upatikanaji wa taarifa, ushiriki katika ufanyaji maamuzi na uwajibikaji wa kuchukua hatua hasa wakati huu ambapo dunia inakabiliana na janga la corona au COVID-19.  Jason Nyakundi na maelezo zaidi.

 Kupitia ujumbe wake wa siku hii Guterres amesema hata hivyo tangu mwanzo wa janga hili dunia imeshuhudia dharura hiyo ikitumika katika nchi nyingi kubinya mchakato wa demokrasia na majukwaa ya kiraia. Ameongeza kuwa "Hii ni hatari hususan katika maeneo ambako mizizi ya demokrasia ni finyu na mifumo ya ufuatiliaji na uwiano wa tasisi ni dhaifu. Janga hili limeanika wazi suala la kutokuwepo usawa ambalo limepuunzwa kwa muda mrefu, kuanzia mifumo duni ya afya hadi pengo katika hifadhi ya jamii, pengo katika masuala ya kidijitali na kutokuwepo usawa katika fursa za elimu , mmomonyoko wa mazingira hadi ubaguzi wa rangi na ukatili dhidi ya wanawake.” 

Na mbali ya athari kubwa za kibinadamu ,pia amesema  mapengo haya ya usawa yenyewe ni tishio tosha kwa demokrasi. Katibu mkuu amesisitiza kwamba hata kabla ya janga la COVID-19 kiwngo cha watu kuchanganyikiwa sababu ya changamoto za maisha kilikuwa kinaongezeka huku imani kwa malaka ikiendelea kushuka. 

Na ukosefu wa fursa ulichangia kuyumba kwa uchumi na kuleta machafuko katika jamii. Lakini leo hii amesema "Ni bayana kwamba serikali ni lazima ziongeze juhudi kuwasikiliza watu wanaodai mabadiliko, kufungua njia mpya kwa ajili ya majadiliano na kuheshimu uhuru wa kukusanyika kwa amani.” 

Katika siku hii ya demokrasia Guterres ameichagiza dunia kutumia fursa hii muhimu kujenga dunia endelevu yenye usawa zaidi, jumuishi, na inayoheshimu haki za binadamu. 

 

 

  

Audio Credit
Flora Nducha/Jason Nyakundi
Audio Duration
1'48"
Photo Credit
Photo: UNDP Madagascar