Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

DRC Shule zikifunguliwa, dawati moja mwanafunzi 1 ili kuepusha COVID-19

DRC Shule zikifunguliwa, dawati moja mwanafunzi 1 ili kuepusha COVID-19

Pakua

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC imeitikia wito wa Umoja wa Mataifa wa kufungua shule ili wanafunzi wanaofanya mitihani yao ya kuhitimu elimu ya msingi na sekondari waweze kuendelea masomo yao licha ya kuwepo kwa janga la ugonjwa wa virusi vya Corona, COVID-19 katika maeneo mbalimbali duniani ikiwemo taifa hilo la maziwa makuu. Ahimidiwe Olotu na taarifa zaidi.

Shule zimefunguliwa mwezi uliopita huku mamlaka zikizingatia kanuni zilizopendekezwa na shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO, la kuhakikisha kuna huduma za kujisafi ikiwemo maji ya kunawa mikono na sabuni sambamba na umbali wa mita mbili kati ya wanafunzi iwe ni darasani au wakati wa michezo.

Miongoni mwa shule ambazo zinazingatia kanuni hizo ni shule ya msingi ya Tobongisa iliyopo mji mkuu wa DRC, Kinshasa ambako wanafunzi wanavaa barakoa na kunawa mikono mara kwa mara sambamba na kuheshimu umbali wa kutochangamana ili kuepusha maambukizi ya virusi vya Corona ambavyo hadi sasa havina tiba wala chanjo.

Hatua zilizochukuliwa

Video ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, inamfuatilia mwanafunzi mmoja aitwaye Lovely tangu anapoondoka nyumbani kwao asubuhi kuelekea shuleni.

Darasani dawati moja lina mwanafunzi mmoja na kila mwanafunzi akiwemo Lovely, amevalia barakoa yake.

Elimu ya jinsi ya kujikinga na COVID-19 inaendelea pia darasani ambako wanafunzi wanaonekana wakiimba wimbo huku wakionesha vitendo vya kunawa mikono kwa sabuni kwa sekunde 20 hadi mikono inapokuwa misafi.

Wakati wa mapumziko, mwalimu anahakikisha kuwa umbali wa kutochangamana unazingatiwa na wanafunzi wote wanakuwa salama ili waweze kufanya mitihani yao ya kumaliza elimu ya msingi na sekondari.

Wanafunzi wakiwa darasani nchini DRC,  akiwemo Lovely, (wa 2 kutoka kushoto) na pia wananawa mikono yao mara kwa mara.
UNICEF/Josue Mulala
Wanafunzi wakiwa darasani nchini DRC, akiwemo Lovely, (wa 2 kutoka kushoto) na pia wananawa mikono yao mara kwa mara.

 

Maoni ya mwanafunzi wa Kinshasa

Akizungumzia hatua hii ya kurejea shuleni Lovely anasema ”ni kweli nimefurahia sana kurejea shuleni kwa sababu nyumbani nilikuwa sifurahii kwa kuwa sikuwa nawaona marafiki zangu, walimu wangu lakini unapokuwa shuleni hali hiyo imebadilika. Hapa tunatakiwa tuvae barakoa wakati wote tukiwa darasani na tukiwa tunacheza. Kila darasa lina sehemu ya kunawa mikono.”

Mwanafunzi Lovely akafafanua jinsi ya mkao kwenye darasa akisema, “kwa wanafunzi wote wa darasa la 6 awali walikuwa wanaketi wawili au watatu kwenye dawati moja lakini sasa hivi ili kuzingatia mbinu za kutochangamana, kuna mgawanyo kwenye madarasa. Kila darasa lina wanafunzi 20 na kila dawati mwanafunzi mmoja. Na nyumbani najiandaa kwa mitihani yangu kwa kusoma na kufuatilia masomo kwenye redio. Kwa wanafunzi wenzangu wanaojiandaa kwa mitihani wakiwa nyumbani au shuleni kutokana na janga hili, nawasihi wazingatie mbinu za kutochangamana na nawatakia.Nawatakia wanafunzi wa darasa la sita mtihani mwema.”

Kwa mujibu wa takwimu za shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO, DRC hadi sasa ina wagonjwa 10,360 waliothibitishwa kuwa na COVID-19 na kati yao hao 260 ndio wamefariki dunia.

Audio Credit
Flora Nducha/Ahimidiwe Olotu
Audio Duration
1'55"
Photo Credit
UNICEF/Josue Mulala