Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNMISS yaeleza kuwa watu 135,000 wametawanywa na mafuriko Bor wengine wapoteza kila kitu

UNMISS yaeleza kuwa watu 135,000 wametawanywa na mafuriko Bor wengine wapoteza kila kitu

Pakua

Watu 135,000 wametawanywa na mafuriko katika eneo la Bor na Twic kwenye jimbo la Jonglei nchini Sudan Kusini huku wengine wakipoteza kila kitu kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini humo. Jason Nyakundi na maelezo zaidi.

Katika mitaa ya Bor Sudan Kusini hali ni dhahiri kwamba mafuriko hayo ni makubwa, kina mama kina baba na watoto wanajaribu kunusuru chochote kinachowezekana wakiwa na vifurushi kichwani ikiwemo magodoro na vifaa vya nyumbani.

Kwa mujibu wa mpango wa Umoja wa Mataifa nchini humo UNMISS, wengi wamepoteza kila kitu katika mafuriko hayo ambayo pia yamesomba nyumba na kuharibu miundombinu ikiwemo barabara.

David Garang Goch ni mwanaharakati wa asasi za kiraia kwenye eneo la Bor, “watu wametaharuki kwa kutokujua wapi watakapokwenda kulala leo. Maji ni mengi kiasi kwamba watu wanashindwa hata kuweka kingo za kuyazuia maji. Hali ni mbaya sana na watoto, wanawake na wazee ndio waathirika wakubwa wa mafuriko haya.

Kila mtu anajitahidi kadri awezavyo kuhakikisha anaokoa chochote iwe ni biashara au nyumba zao kutosomwa na mafuriko hayo.

Gavana wa jimbo la Jonglei Denay Chagor anasema matatizo ni mengi na yako kila kona na hili ni janga la kitaifa ni tishio ambalo si kubwa kama vita lakini ni janga linalohitaji kushughulikiwa haraka.

Na wito huo umeitikiwa na mpango wa Umoja wa Mataifa UNMISS, sasa kikosi cha wahandisi wa UNMISS kutoka Korea kimekuwa kikishirikiana na jamii kunusuru kinachowezekana likiwemo soko na hospitali pekee ya Jonglei ili visisombwe na maji.

Soko la Marol ndio tegemeo pekee la wafanyabiashara na jamii ya eneo hilo. Mkuu wa ofisi ya UNMISS Jonglei Debrorah Schein anasema,“tunashukuru kwamba hizi ni juhudi za pamoja , ukiangalia utaona wanajamii wanaweka viroba vya mchanga kuzunguka maduka yao, wameyafunga na mbele ya maduka hayo wameweka viroba vya nchanga, kila mtu anaweka viroba kukinga maji na wanafanya hivyo kwa mikono yao, watoto, wanawake wote, wanaume wote , kila mtu wanashirikiana.”

Nyumba nyingi zimebomolewa na mafuriko hayo na zilizobaki sasa ni mahame watu wamekimbia kwenda kusaka mahala salama pa kujihifadhi.

 

Audio Credit
Assumpta Massoi/Jason Nyakundi
Audio Duration
2'21"
Photo Credit
Video Screen Shot