Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uchaguzi ufanyike kwa amani-Raia wa CAR 

Uchaguzi ufanyike kwa amani-Raia wa CAR 

Pakua

Kuelekea uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR tarehe 27  mwezi Desemba mwaka huu, wapiga kura kwenye mji mkuu wa nchi hiyo, Bangui wametoa maoni yao wakati huu ambapo tayari kazi ya kuandikisha wapiga kura ilianza mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu. Flora Nducha na ufafanuzi zaidi.

Wapiga kura hao wakihojiwa na Radio Guira FM ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini CAR, MINUSCA wamesema, “ni wakati wa kila mwana CAR kupima thamani ya kila mgombea ambaye anataka kuongoza mustakabali wao. Kwa hiyo tunapenda chaguzi hizo zifanyike kwa utulivu na amani.” 

Kwa mkazi mwingine wa Bangui suala muhimu ni uchaguzi uwe huru akisema, “ni kuwaachia wana Jamhuri ya Afrika ya Kati wapige kura kwa uhuru na tuzingatie matokeo ya chaguzi hizo na kati wasituchagulie mtu ili kipindi cha uchaguzi kiweze kupita salama.” 

Wagombea nao wakapatiwa wito na mkazi mwingine wa Bangui ambaye yeye anasema, “natoa wito kwa wote, wapiga kura, wagombea n apande zote, tukumbuke kuwa sote tu wananchi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati. Sote tunakwenda kwenye uchaguzi na vita havitusongeshi popote. Tufanye chaguzi kwa amani na tuendelee kuishi kwa amani.” 

Katika miezi ya hivi karibuni, nyaraka na vifaa vya uchaguzi viliwasili nchini humo ikiwemo kompyuta ndogo za dijitali 4,400 kwa ajili ya kuandikisha wapiga kura, vibanda vya kupigia kura, paneli za sola na betri pamoja na vifaa vya kuhifadhi umeme na vifaa vyote hivyo vimesambazwa kote nchini CAR kwa usaidizi wa MINUSCA. 

Azimio la Baraza la Usalama la  Umoja wa Mataifa namba 2499 linapatia MINUSCA jukumu la kusaidia mamlaka za CAR katika maandalizi na kufanyika salama kwa uchaguzi huo ujao. 

Kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi, iwapo katika awamu ya kwanza ya uchaguzi war ais tarehe 27 mwezi huu hakutakuwa na mshindi anayepata zaidi ya asilimia 50 ya kura zitakazopigwa, basi awamu ya pili itafanyika tarehe 14 mwezi Februari mwaka 2021. 

Uchaguzi mkuu wa mwisho ulifanyika nchini humo mwaka 2015/2016. 

 

Audio Credit
Flora Nducha
Audio Duration
2'16"
Photo Credit
UN photo / Catianne Tijerina