Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkulima Ethiopia: IFAD imetuwezesha kujenga nyumba na kulala kwenye vitanda

Mkulima Ethiopia: IFAD imetuwezesha kujenga nyumba na kulala kwenye vitanda

Pakua

Nchini Ethiopia, mradi wa umwagiliaji maji mazao uliofanikishwa na mfuko wa Umoja wa Mataifa wa maendeleo ya chakula na kilimo, IFAD, umeleta nuru kwa wakulima na hata wengine kuweza siyo tu kujenga nyumba kwa mara ya kwanza, bali pia kulala kwenye kitanda na kupatia familia zao milo mitatu. Ahimidiwe Olotu na maelezo zaidi.

IFAD inasema kuwa ingawa dunia inaripotiwa kuwa na kiwango kikubwa cha maji, bado maji hayo hayapatikani katika maeneo yanakotakiwa na kwa wakati unaotakiwa. 

Mathalani nchini Ethiopia, taifa lililozoeleka kuwa na ukame na njaa, mabadiliko ya tabianchi yamefanya vipindi vya ukame kuwa virefu zaidi na kuleta madhara makubwa kwa wakulima wadogo wadogo vijijini. 

Miongoni mwao ni Molach Belay Abay, anayeishi na kulima huko eneo la Tigray ambako kutokana na uhaba wa maji wa muda mrefu hakuweza kumwagilia mazao na hivyo kushindwa kuuza mazao kupata kipato na kulisha familia yake ya watoto wanne. 

“Hapo zamani kulikuwa na umaskini wa kupindukia. Tulikuwa na matatizo makubwa kwa kuwa kipato chetu kilitokana na kilimo. Tuliuza mazao na fedha zikawa kwa matumizi yetu ya kulipia watoto shule, kununua pilipili na chumvi, na ikifika mwezi Juni na Julai fedha yote imekwisha,”  anasema Molach.  

Hata hivyo ili kuhakikisha wakulima wanakuwa na kipato mwaka mzima, IFAD ilipatia fedha serikali ya Ethiopia ili kujenga bwawa na mifumo midogo ya umwagiliaji maji. 

Mradi huo unapatia mafunzo pia wakulima ili waweze kulima siyo tu wakati wa ukame lakini pia mazao tofauti yenye lishe. 

Molach anasema, “kutokana na umwagiliaji tuliweza kuvuna matunda, na aina mbalimbali za mboga. Sisi wanawake ambao awali hatukuwa na ajira wala elimu sasa tuna ufahamu.” 

Girmachew Tardesse ni mtaalamu wa mradi huo PASIDPII na anasema ya kwamba, “IFAD inasaidia wakulima kuwa na kipato cha ziada hata na kipande kidogo cha ardhi walicho nacho, wanapata fedha zaidi kwa kupata aina mbalimbali za mazao yenye faida kiuchumi.” 

IFAD inasema kutokana na kuwa na aina mbalimbali za mazao kwa ajili ya kuuza, sasa maisha ya Molach na familia yake yamebadilika mwenyewe akisema, “ sasa tunajitegemea. Unaona hii nyumba hapa niliposimama, ni sisi tumejenga, na sasa tunalala kitandani. Tumepata fursa ambazo wazazi wetu hawakupata. Nalisha wanangu mara 4 kwa siku.” 

PASIDP II imebadili maisha ya wakulima 62,000, mradi ambao ulianza kwa kuongeza kiambato kimoja tu ambacho ni upatikanaji wa maji mwaka mzima. 

 

Audio Credit
Flora Nducha/Ahimidiwe Olotu
Audio Duration
1'55"
Photo Credit
© UNICEF/Tanya Bindra