Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuwa mkimbizi bila kazi Lebanon ni mtihani mkubwa: Mkimbizi Ibrahim

Kuwa mkimbizi bila kazi Lebanon ni mtihani mkubwa: Mkimbizi Ibrahim

Pakua

Kutana na mkimbizi Khalili Ibrahim kutoka Syria ambaye ajali na athari za janga la corona au COVID-19 ilimlazimisha kumwachisha binti yake shule ili afanye kazi taarifa zaidi na Jason Nyakundi

Mjini Beiruti nchini Lebanon mkimbizi Khalil Ibrahim kutoka Syria akiwa ndani ya hema lake na familia yake kwenye makazi ya wakimbizi ya Tripoli. Miongoni mwa wanafamilia hao ni binti yake Nahid mwenye umri wa miaka 12. 

Baada ya kupata ajali na kuumia vibaya kazini Khalil ilibidi aache kazi na hakuwa na jinsi bali kuzalimika kumwachisha binti yake shule ili akafanye kazi ya msimu wa mavuno pamoja na mama yake ili kuweza kusaidia kumudu mahitaji ya familia uamuzi ambao umemuumiza sana Khalil Nilimtoa binti yangu shule kwa sababu tunaishi katika mazingira ambayo siwezi kueleza. Kodi, bili ya umeme, maji vyote hivi tunapaswa kulipa kila mwisho wa mwezi na siwezi kumudu” 

Khalil anasema kuishi ukimbizini tena bila kazi inayoingiza kipato ni mtihani mkubwa na sababu ya ajali aliyopata sasa familia imelimbikiza deni la dola 1000. Mkewe Mona na bitiye Nahid wanalipwa ujira wa jumla ya chini ya dola 2 kwa siku na hatua za kupambana na corona inaamanisha sasa saa za kufanya kazi ni chache . 

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limeongeza msaada wa fedha kwa wakimbizi tangu kuzuka kwa janga la COVID-19 na kudorora kwa uchumi lakini mahitaji yanaendelea kupita msaada wanaopewa. 

Kamishina Mkuu wa wakimbizi Filippo Grandi amehitimisha ziara yake mwishoni mwa wiki nchini Lebanon ambako alipata pia fursa ya kuwatembelea wakimbizi eneo la Tripoli na bonde la Bekaa na kusikiliza kilio chao na familia ya Khalil ni miongoni mwa waliobahatika kutembelewa alipozungumza nao Grandi akasema “Sisi pamoja na shirika la mpango wa chakula duniani  WFP, UNICEF na mashirika mengine mengi yasiyo ya kiserikali NGO’s tunafanyakazi Pamoja na serikali ya Lebanon pia na wakimbizi kujaribu kusaidia katika kiwango cha kibinadamu, angalau kukidhi mahitaji ya kipindi hiki kigumu.” 

Matumaini ya Khalil ni kwamba siku moja binti yake atazishuhudia siku za furaha na kuweza kuendelea na shule. 

Na kwa UNHCR inasema katika miezi ya karibuni kutokana na athari za COVID-19 za kiuchumi na kijamii idadi ya wakimbizi wanaoishi katika umasikini uliokithiri imeongezeka kutoka asilimia 55 hadi zaidi ya asilimia 75 leo hii. 

Audio Credit
Flora Nducha/Jason Nyakundi
Audio Duration
2'32"
Photo Credit
UNICEF/UN0277723/Souleiman