Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19: Takribani mtoto 1 kati ya 3 ya watoto wa shule duniani kote, hakuweza kupata masomo nje ya mazingira ya shule-Ripoti 

COVID-19: Takribani mtoto 1 kati ya 3 ya watoto wa shule duniani kote, hakuweza kupata masomo nje ya mazingira ya shule-Ripoti 

Pakua

Ripoti mpya ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF iliyotolewa hii leo mjini New York Marekani imeeleza kuwa takribani theluthi moja ya watoto wote wa shule duniani, yaani watoto milioni 463 hawakuweza kupata masomo wakiwa nyumbani wakati COVID-19 iliposababisha kufungwa kwa shule. Taarifa Zaidi na Ahimidiwe Olotu

Akizungumzia ripoti hiyo ambayo imetoka katika nyakati ambazo nchi mbalimbali zinakabiliana na mipango yake ya kuzifungua shule, Mkurugenzi Mkuu wa UNICEF Bi Henrietha Fore amesema, “kwa watoto takribani milioni 463 ambao shule zao zilifungwa kutokana na COVID-19, hakukuwa na kitu kama kusomea nyumbani. Idadi kubwa ambayo ilisambaratika kwa miezi mingi, ni dharura ya ulimwengu. Athari zinaweza kuonekana katika uchumi wa jamii kwa miongo kadhaa ijayo.” 

Ripoti inasema kuwa kwa ngazi ya nchi kufungwa na pia mazuio ya kutembea, takribani watoto wa shule bilioni 1.5 waliathiriwa na kufungwa kwa shule. Ripoti hiyo inaeleza mapungufu ya masomo nje ya shule na kufichua ukosefu wa mkubwa wa usawa katika ufikiaji wa masomo.   

Ripoti hiyo ya UNICEF inatumia uchambuzi wa tathimini ya ulimwengu kutoka nchi 100 kuhusu upatikanaji wa teknolojia nyumbani na zana zinazohitajika kwa ujifunzaji wa nje ya shule za awali, msingi, na sekondari. Takwimu zilizotumika zinajumuisha televisheni, redio na intaneti na pia uwepo wa mtaala unaoweza kusambazwa kupitia njia hizi wakati shule zimefungwa. 

Ingawa takwimu katika ripoti tayari zinaonesha hali ya wasiwasi kuhusu uhaba wa kujifunza nje ya shule wakati shule zimefungwa, UNICEF inatahadharisha pengine hali ni mbaya zaidi. UNICEF inasema hata pale ambapo watoto wana teknolojia na zana majumbani, wanaweza wasiweze kujifunza nje ya shule kupitia vifaa hivyo kutokana na sababu kadhaa majumbani ikiwemo kazi za nyumbani, kulazimishwa kufanya kazi, mazingira duni ya kusoma na ukosefu wa usaidizi katika kutumia mtaala na matangazo ya mtandaoni. 

Ukanda Mashariki na Kusini mwa Afrika, hali ni mbaya zaidi 

Ripoti inaonesha hali ya kukosekana kwa usawa katika kanda zote. Watoto wa shule katika ukanda wa kusini mwa jangwa la Sahara ndio walioathirika zaidi ambapo nusu ya wanafunzi wote hawawezi kufikiwa na masomo ua nje ya shule zao.  Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika imeonesha takribani asilimia 49 sawa na watoto milioni 67 hawawezi kupata masomo wakiwa nje ya shule. 

 

Aidha ripoti hiyo inasema watoto wa shule kutoka katika kaya maskini na wale wanaoishi vijijini wako hatarini zaidi kukosa masomo wakati wa kufungwa kwa shule. Duniani kote, robo tatu ya watoto wa shule ambao hawawezi kupata masomo nje ya shule, wanaishi vijijini.  

UNICEF inahimiza serikali kuweka kipaumbele katika kufunguliwa upya kwa shule wakati nchi hizo zinapoanza kupunguza  vikwazo. Na pale ambapo kufungua shule hakuwezekani, UNICEF inahimiza serikali kuingiza masomo ya kufidia muda uliopotea katika mipango ya ufunguaji upya wa shule. 

Audio Credit
Flora Nducha/Ahimidiwe Olotu
Audio Duration
2'14"
Photo Credit
UNICEF/Habib Kanobana