Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP yaelekeza meli yake yenye shehena za vyakula Lebanon ili kunusuru wananchi

WFP yaelekeza meli yake yenye shehena za vyakula Lebanon ili kunusuru wananchi

Pakua

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani, WFP limefikisha tani 12,500 za unga wa ngano nchini Lebanon ili kuepusha ongezeko la bei ya mkate nchini humo kwa mwezi wote wa Septemba unaoweza kusababishwa na milipuko mikubwa ya tarehe 4 mwezi huu wa Agosti iliyosambaratisha bandari ya Beirut ambayo ni tegemeo kwa kupokea shehena za mizigo katika taifa hilo la Mashariki ya Kati. Assumpta Massoi na maelezo zaidi. 

Bandari ya Beirut nchini Lebanon, shehena ya ngano ikipakiwa kwenye malori ya shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani, WFP tayari kusambazwa kwa wahitaji wakati huu ambapo kuna hofu kuwa bei ya mkate, tegemeo kuu nchini humo itaongezeka kufuatia milipuko Beirut. 

Upakiaji ukiendelea wafanyakazi wa WFP wanajenga bohari mpya ya kuhifadhia shehena nyingine, kulikoni? Amer Daoudi ni Mkurugenzi wa Operesheni za WFP nchini Lebanon. “Maeneo yote ya kuhifadhi nafaka yameharibiwa. Vinu vyote vya kuhifadhia nafaka vimeharibiwa. Hapa ni eneo pekee katika Lebanon nzima ambalo lina uwezo wa kupokea shehena kubwa na nyingi ya nafaka, iwe ni kwa ajili ya kutengeneza mikate au chakula cha mifugo. Eneo la kuhifadhi limeharibiwa kabisa. Mifumo yote ya kupakua na kupakia imesambaratishwa. Kile ambacho WFP imefanya katika siku chache ni kuelekeza meli yake yenye tani 12,500 kufika hapa ili kusaidia wananchi wa Lebanon na kuhamasisha ujenzi wa hifadhi mpya hapa nilipo unaona nyuma yangu wanajenga na tuko kwenye mchakato wa kuongeza uwezo wa bandari ya Beirut ili iweze kushughulikia shehena nyingi.” 

Kwa wakazi wa eneo la Karantina lililo jirani na bandari ya Beirut, milipuko iliharibu kwa kiasi kikubwa makazi yao. 

Miongoni mwa wakazi hao ni Omar Hussein ambaye ni kibarua na siku ya mlipuko, alijikuta amerushwa hadi ardhini na kufunikwa na vifusi vya vioo vilivyovunjika na maisha yake na familia yake ni ya taabu. “Hata kabla ya milipuko, hali ilikuwa mbayá sana. Mimi na mke wangu tunahitaji dawa zinazogharimu dola 560 na hatuna msaada zaidi ya Mungu. Watoto wetu walikuwa wanatusaidia hadi dola 46, lakini baada ya maandamano na kuenea kwa ugonjwa wa virusi vya Corona, COVID-19, hawana tena ajira. Hii imetufanya tupitishe takribani miezi 2 bila dawa.” 

Sasa tegemeo lao ni msaada wa chakula kutoka WFP ambapo familia 200 zimepatiwa msaada wa chakula. 

WFP inakadiria kuwa ili kukidhi msaada wake wa dharura Lebanon, linahitaji dola milioni 235 kwa miezi 6 ijayo ili liweze kusambaza chakula kwa walio na uhitaji zaidi. 

Audio Credit
Flora Nducha\Assumpta Massoi
Audio Duration
2'37"
Photo Credit
WFP/Malak Jaafar