Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID 19 imeathiri utalii na hivyo kuharibu ajira, uchumi na urithi wa asili-Guterres

COVID 19 imeathiri utalii na hivyo kuharibu ajira, uchumi na urithi wa asili-Guterres

Pakua

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia tamko lake la kisera kuhusu utalii na COVID-19, amesema imeleta maumivu makali kuona jinsi ambavyo utalii umeharibiwa na janga la COVID-19. 

Bwana Guterres akizungumza kwa njia ya video amesema utalii ni miongoni mwa sekta muhimu zaidi ulimwenguni na sekta hiyo inatoa ajira kwa mtu mmoja katika kila watu kumi duniani huku ikitoa riziki kwa mamilioni zaidi ya watu. “Inakuza uchumi na kuwezesha nchi kustawi. Inaruhusu watu kuendeleza utajiri wa kitamaduni na asili na kuwaunganisha watu na kuonyesha utu wetu. Kwa kweli, mtu anaweza kusema kuwa utalii wenyewe ni moja ya maajabu ya ulimwengu. Ndio maana imeleta maumivu makali kuona jinsi ambavyo utalii umeharibiwa na janga la COVID-19.”  

 Aidha Bwana Guterres amesema katika miezi mitano ya mwanzo wa mwaka huu wa 2020, zaidi ya nusu ya watalii wanaowasili kimataifa walipungua na hivyo dola bilioni 320 katika mauzo ya nje kutokana na utalii zimepotea. 

Baada ya kueleza namna ambavyo COVID-19 imeuathiri utalii kote duniani ameeleza maeneo matano ambayo ameyaanisha kuwa ni maeneo ya kipaumbele ili kusaidia hali kurejea kusimama upya.  

“Kwanza, kupunguza athari za kiuchumi na kijamii zitokanazo na janga hili. Pili, kujenga ustahimilivu katika mnyororo wa thamani kwenye utalii.Tatu, kuongeza utumiaji wa teknolojia katika tasnia ya utalii. Nne, kukuza uendelevu na ukuaji imara. Na ya tano, kukuza ushirikiano ili kuwezesha utalii kusaidia zaidi Malengo ya Maendeleo Endelevu.Tuhakikishe utalii unarejea tena kwenye nafasi yake kama mtoaji wa ajira,kipato thabiti na ulinzi wa urithi wetu wa kitamaduni na asili.Asante.” 

Audio Credit
Flora Nducha
Sauti
1'50"
Photo Credit
World Bank/Curt Carnemark