Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Furaha yetu ni kupata majawabu Lamu bila urasimu - Umra

Furaha yetu ni kupata majawabu Lamu bila urasimu - Umra

Pakua

Katika maeneo ya ndani zaidi ya kaunti ya Lamu, kaskazini mashariki mwa pwani ya Kenya, huduma za afya zinakumbwa na changamoto kubwa. Ni kwa mantiki hiyo kila mwezi madaktari na wafanyakazi wa shirika la kiraia la Safari Doctors hufunga safari kwa boti, wakiwa na shehena za dawa kwa ajili ya kutibu siyo tu binadamu bali pia wanyama. Safari  Doctors imeasisiwa na Umra Omar ambaye pia ndiye Mkurugenzi na pia miongoni mwa mashujaa halisi wa kibinadamu wa Umoja wa Mataifa kwa mwaka huu wa 2020.

Licha ya ukosefu wa usalama kwenye maeneo ya mpaka wa kaunti hiyo na Somalia, sambamba na vitisho vitokanavyo na ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19, Safari Doctors wameendelea na kazi yao adhimu kila mwezi wakitembelea vijiji vilivyo pembezoni huko Lamu.

Akielezea simulizi yake, Bi. Omar anasema kwamba “mimi natoka kisiwa cha Pate kwenye kaunti ya Lamu. Nimepata shahada yangu ya pili kutoka nchini Marekani na nimefanya kazi Washington D.C nchini Marekani, lakini niliamua kurejea nyumbani mwaka 2015 na kuanzisha Safari Doctors.”

Nchini Kenya, asilimia 70 ya wananchi wanaishi maeneo ya ndani ambako huduma ya afya si rahisi na nafuu na ni vigumu kwa wagonjwa kufika hospitalini “ndio maana tuliamua kuanzisha Safari Doctors,”  anasema Bi. Omar.

Kwa Safari Doctors, kupata dawa kwa ajili ya wagonjwa ilikuwa rahisi kwa kuwa tayari zinapatikana, changamoto ikawa ni jinsi ya kufikisha dawa hizo kwa wahitaji. “Ilinibidi nibonge bongo jinsi ya kuchangisha dola 500 kwa mwezi, kwa ajili ya kumlipa muuguzi na mafuta ya pikipiki. Nilifanya hivyo kwa mwaka mzima. Mwaka uliofuata, tuliongeza vijiji zaidi na kupata kutambulika zaidi, hasa pale tuliposhinda tuzo  kutoka shirika la utangazaji la CNN.”

Jamii iliyo hatarini kupata janga

Kwa wakazi wa Lamu, janga la COVID-19 limeongeza chumvi kwenye kidonda na hivyo kufanya kazi ya Safari Doctors kuwa ya muhimu zaidi.

Kati ya mwezi Machi na Juni mwaka huu, timu ya Safari Doctors ilitembelea visiwa vya Lamu kwa boti na kutibu zaidi ya wagonjwa 4000 katika vijiji 17, wagonjwa ambao bila ujio wa madaktari hawa hali yao ingalikuwa vinginevyo.
“Pia tuna programu ya kutibu mifugo iitwayo Safari Vet ambayo imetibu zaidi ya wanyama 400 katika kipindi hicho hicho, huku wakieleza umuhimu wa kuzuia kuenea kwa magonjwa ya wanyama kwenye kwa binadamu, chanzo cha virusi vya COVID-19, hali ambayo inatukumbusha kuwa afya ya binadamu ina uhusiano na afya ya wanyama na mazingira.”

Kuwekeza kwa vijana

Tulibaini alikuwa na uvimbe shingoni na baada ya kuchunguza ilikuwa ni risasi; alikuwa amepigwa risasi miaka miwili iliyopita wakati kijiji chao kiliposhambuliwa. Umra Omar - Muasisi  Safari Doctors

Bi. Omar anasema kuwa kila wakati amekuwa akiandamana na timu yake wanapokwenda vijijini au kwenye eneo ambalo halina usalama. “Timu yetu bado ni ya vijana sana. Mimi ndiye mwenye umri mkubwa zaidi ambao ni miaka 37. Pindi mashirika mengine yanapoondoa timu zao wakati wa majanga kama vile janga la sasa la COVID-19, sisi tunasalia. Tumeanzisha programu ya mabalozi vijana wa afya; haw ani vijana wa kujitolea katika masuala ya kibinadamu wakiwa katika vijiji vyao,”  amesema muasisi huyo wa Safari Doctors.

Furaha yetu ni pale tupatapo majawabu bila urasimu

Kwa Bi.Omar, kitendo cha Safari Doctors kuweza kufanya kazi katika ngazi ya jamii na kuona masuala muhimu yakichukuliwa hatua papo kwa papo badala ya kusubiri urasimu ni jambo muhimu sana, “na kwa sababu ya mawasiliano yetu tunaweza kuwa na mtandao hadi ngazi za kimataifa.”

Anatoa mfano kuwa “siku moja, pindi wageni wetu walitutembelea kutoka Marekani, tulikutana na mwanamke mmoja akilalamika maumivu ya kichwa. Tulibaini kuwa alikuwa na uvimbe shingoni na baada ya kuchunguza ilikuwa ni risasi; alikuwa amepigwa risasi miaka miwili iliyopita wakati kijiji chao kiliposhambuliwa.”

Bi. Omar anasema kwa sababu ya mtandao wao waliweza kupata ndege iliyomsafirisha hadi hospitali kwa ajili ya matibabu. Anasema hicho ni kisa kimoja tu, lakini ilitosheleza kuona kuwa waliweza kufanya uamuzi haraka bila urasimu.

Na akihitimisha, Umra Omar anasema kuwa, “tunapaswa kuacha kuwa na mtazamo kuwa kazi ya kiutu ni suala la kusherehekewa, bali linapaswa  kuwa jambo la kawaida. Hili ndio lengo la Safari Doctors. Na hii ndio maana tunaweka uwekezaji zaidi kwenye ushiriki wa rai ana uongozi wa vijana.”

Audio Credit
Flora Nducha
Audio Duration
1'42"
Photo Credit
Safari Doctors