Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nilichokiona Beirut sitosahau katu -Mkimbizi wa Syria

Nilichokiona Beirut sitosahau katu -Mkimbizi wa Syria

Pakua

Nchini Lebanon, wakimbizi kutoka Syria walionusurika katika mlipuko mkubwa wa tarehe 4 mwezi huu wa Agosti kwenye mji mkuu wa Lebanon, Beirut wamesimulia kile ambacho walishuhudia na kiwewe kilichowakumba katika tukio hilo lililosababisha vifo vya watu zaidi ya 170 na wengine zaidi ya 6500 wamejeruhiwa. Assumpta Massoi na maelezo zaidi. 

Taswira kutoka angani ya uharibifu mkubwa kwenye bandari ya Beirut nchini Lebanon, majengo yamesalia magofu, vifusi vya vioo na matofali. 

Taswira hii imesalia kwenye fikra za wakimbizi kutoka Hakassah nchini Syria ambao sasa ni wakazi wa Beirut. 

Aisha akiwa amekumbatia wanae wawili wa kiume, Zakarya na Yahya, wote watatu wakiwa wamefungwa bandeji kutokana na majeraha ya Agosti 4 anasema walisikia kishindo wakadhani ni ndege na walipochungulia dirishani kila kitu kilisambaratika na zaidi ya yote.“Kushuhudia mtoto wangu anavuja damu kichwani na sisi tunashindwa kuizuia, lilikuwa ni jambo gumu sana. Nami sikuwa na habari kuwa nilikuwa nimejeruhiwa.” 

Mumewe Aisha aitwaye Ahmed aliposikia kishindo aliwafuata lakini kabla hajawafikia, madirisha yote na vioo vikawaangukia na kuwafunika Aisha na wanae wawili. “Ni kitu ambacho sijawahi kukihisi awali. Nilidhani nyumba yote imelipuka. Sikuweza kuona chochote. Vumbi lilijaa kila kona. Nilimsikia mume wangu akipaza sauti, Aisha! Mungu wangu, Mungu wangu! Yahya, Zakariya!” 

Familia hii inasema kuwa machungu wanayopitia na kile walichoshuhudia kitasalia kwenye fikra na miili yao kwa muda mrefu. 

Audio Credit
Flora Nducha/Assumpta Massoi
Audio Duration
1'47"
Photo Credit
Houssam Yaacoub