Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kwa wasiojua kusoma, michoro kwenye kuta CAR ni jawabu katika kujikinga na COVID-19

Kwa wasiojua kusoma, michoro kwenye kuta CAR ni jawabu katika kujikinga na COVID-19

Pakua

Nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu, MINUSCA umeshirikiana na serikali kuchora picha za kuelimisha watu jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19 ambao hadi sasa nchini humo umesababisha vifo vya watu 61 miongoni mwa wagonjwa 4,652 waliothibitishwa. Assumpta Massoi anaeleza zaidi.

Michoro hiyo katika mji mkuu wa CAR, Bangui pamoja na kuonesha dalili za COVID-19, pia inaonesha unyanyapaa na mbinu za kujikinga.

Philippe Boukola ni Mkurugenzi wa Sanaa na Utamaduni katika Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Utalii nchini CAR na anasema kuwa, "idadi kubwa ya wananchi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati hawajui kusoma na kuandika. Kile tunachoandika ni kwa wale wanaofahamu kusoma, lakini sentensi kwenye picha inasaidia wasiojua kusoma kuweza kuona ujumbe kupitia picha zilizochorwa na wasanii. Kwa hiyo ni kwa ajili ya kuona ni mambo yapi hupaswi kufanya ili kuepusha kuenea kwa virusi vya Corona."

Michoro imekuwa ni kivutio kwa wapita njia akiwemo Dinkpeng Bessek ambaye anasema kuwa, "ni njia ya mawasiliano, tunamuona mwanamke na mwanae wa kiume na wamevaa barakoa, na hii inatukumbusha mbinu za kujikinga na COVID-19 ambalo ni janga linalotesa hivi sasa."

Mchoro ukionesha muuza pombe ya kienyeji akiwa amevalia barakoa ili kuepusha kuenea kwa virusi vya COVID-19.
MINUSCA/Screenshot
Mchoro ukionesha muuza pombe ya kienyeji akiwa amevalia barakoa ili kuepusha kuenea kwa virusi vya COVID-19.

Picha 14 zimechorwa katika takribani kuta 20 mjini Bangui, ambapo Biliaminour Agnide Alao, Mkuu wa mawasiliano MINUSCA anasema kuwa ni jambo muhimu kwa kuwa wasanii wanaonesha uwezo wao wa kuelimisha kupitia michoro.

Uchoraji pia umefanyika katika kitongoji cha Begoua, kilichopo takribani kilomita 12 kutoka Bangui, ambapo msanii Weangai kupitia mchoro wake anaonesha maisha ya kila siku kwenye eneo hilo na hatua za kujikinga.

Weangai anasema kuwa, "michoro yangu ni kile ninaonacho kijijini. Hivyo anatumia uwezo wake kuonesha kile ambacho kinapaswa kufanywa kuheshimu kanuni za kujikinga."

Miongoni mwa wapita njia ni Rosalie ambaye yeye anauza pombe ya kienyeji ya mtende na anasema kuwa "mimi huwaambia wateja wangu waheshimu kanuni za kujikinga na Corona na pia navaa barakoa nikiwa na wateja wangu."

Audio Credit
Flora Nducha/Assumpta Massoi
Audio Duration
1'56"
Photo Credit
MINUSCA/Screenshot