Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakazi wa Lamu Kenya wabadiuli tabia kutokana na COVID-19

Wakazi wa Lamu Kenya wabadiuli tabia kutokana na COVID-19

Pakua

Umra Omar ambaye ni miongoni mwa mashujaa watano wa kiutu kwa mwaka huu wa 2020 ameelezea jinsi janga la ugonjwa wa virusi vya Corona, au COVID-19 limesaidia kusongesha kazi yao ya kupatia tiba wakazi wa kaunti ya Lamu nchini Kenya kupitia shirika la kiraia la Safari Doctors ambalo yeye ni muasisi na pia mkurugenzi. Kutoka Kenya, Jason Nyakundi ana maelezo zaidi.

Safari Doctors ambao husafiri kwa boti hadi visiwa vingine vidogo huko Lamu, hutumia mbinu bunifu ambapo madaktari wa binadamu na wanyama hutoa matibabu kwa takribani vijiji 15 vilivyopo maeneo ya ndani zaidi na kila mwezi hufikia takribani wagonjwa 1,500. Wanyama wanaotibiwa au kupatiwa chanjo dhidi ya magonjwa ni pamoja na mbuzi, kuku na mbwa. 

Siku chache zilizopita, Umra na timu yake walikuwa kwenye moja ya ziara hizo Lamu, wakati huu ambapo Kenya imethibitisha takribani wagonjwa elfu 30 wa Corona huku zaidi ya 470 wamefariki dunia.

Lamu wagonjwa ni takribani 30 ambapo Umra anasema kuwa, "sisi Safari Doctors tumechukua mkakati usio na gharama kubwa wa kuelimisha wananchi kuanzia mwanzoni mwa mwezi Machi, tuliweka mabango ya kuelimisha maeneo muhimu ya kuingia Lamu, tukaweka pia maeneo ya kunawa mikono huku mabalozi wetu vijana wakipita kwenye jamii zao kuhamasisha watu. Pia tulishirikiana na wadau wetu muhimu kuandaa mafunzo kwa wale walio mstari wa mbele." 

Wakazi wa kisiwa cha Manda katika kaunti ya Lamu nchini Kenya wakiwa kwenye foleni wakisubiri huduma za matibabu kutoka kwa wahudumu wa Safari Doctors.
Safari Doctors
Wakazi wa kisiwa cha Manda katika kaunti ya Lamu nchini Kenya wakiwa kwenye foleni wakisubiri huduma za matibabu kutoka kwa wahudumu wa Safari Doctors.

Akizungumzia ni kwa vipi COVID-19 imeathiri shughuli zao huko Lamu, muasisi huyu wa Safari Doctors anasema kuwa, "limeturuhusu kufanya mabadiliko makubwa ni sawa na janga lililoleta faida kwa kuwa imetubidi kuajiri madaktari wawili kuimarisha kitengo chetu cha tiba, kwa sababu awali tulikuwa tunatumia wafanyakazi wa kujitolea, lakini kutokana na vizuizi vya safari na pia hatari ya maambukizi, sasa hivi tuna madaktari wetu. 

Halikadhalika amesema kuwa shughuli ya kutembelea vijiji ambayo awali ilikuwa ni wiki moja sasa ni kwa mwezi mzima ili kuweza kuzingatia kanuni za kuzuia maambukizi ya Corona kama vile kuepusha kuchangamana. 

Umra ameenda mbali zaidi kusema kuwa mikakati ya kujisafi ili kuepusha COVID-19 imekuwa na faida kwa kuwa, "kumekuwepo na mabadiliko makubwa ya tabia kwenye huduma za kunawa na kujisafi na usafi kutokana na COVID-19. Kuna maeneo ambako kuna viwango vidogo vya wagonjwa wa kuhara na milipuko si mikubwa kama ilivyokuwa awali wakati wa msimu mvua." 

Audio Credit
Flora Nducha/Jason Nyakundi
Audio Duration
1'43"
Photo Credit
Safari Doctors