Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shule zikiwa zinaanza kufunguliwa, bado hakuna huduma za kujisafi kujikinga na COVID-19- Ripoti

Shule zikiwa zinaanza kufunguliwa, bado hakuna huduma za kujisafi kujikinga na COVID-19- Ripoti

Pakua

Mjini Mangina jimboni Kivu Kaskazini katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, mtaalamu wa mradi wa huduma za maji, kujisafi na kunawa mikono, WASH kutoka shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF akionesha watoto namna ya kunawa vizuri mikono yao kwa sabuni. 

Huduma hizi ndizo ambazo taarifa ya pamoja iliyotolewa leo huko Geneva, Uswisi na New York, Marekani na mashirika ya Umoja wa Mataifa, lile la kuhudumia watoto, UNICEF na la afya, WHO, yanasema zinakosekana wakati huu shule zinataka kufunguliwa katikati ya janga la COVID-19. 

Kwa mujibu wa ripoti ya mashirika hayo, shule 2 kati ya 5 zilizotafitiwa, hazikuwa na huduma  za msingi za kujisafi mwaka 2019 na idadi ya watoto wanaohusika ni milioni 818 na hivyo wako hatarini kupata Corona na magonjwa mengine ya kuambukiza.“Zaidi ya theluthi moja ya idadi hiyo wako nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara na idadi ya shule zisizo na huduma za kuna mikono ni 7 kati ya 10 na nusu ya hizo hazina huduma za msingi za kujisafi na huduma za maji,” imesema ripoti hiyo. 

Akizungumzia ripoti hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Henrietta Four amesema kuwa, kufungwa kwa shule kote duniani tangu kuingia kwa COVID-19 kumesababisha changamoto za kipekee kwa elimu na ustawi wa watoto, hivyo ni lazima kupatia kipaumbele watoto kujifunza.  

Amesema ina maana kuhakikisha shule ni salama pindi zinapofunguliwa, ikiwemo usafi wa mikono, maji safi na salama ya kunywa na huduma za kujisafi. 

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus amesema, kupata huduma za maji safi, kujisafi na usafi ni muhimu katika kuzuia maambukizi maeneo yote ikiwemo shuleni.

Amesema ni lazima kiwe kipaumbele cha serikali katika mkakati wake wa kufungua na kuendesha shule kwa usalama wakati huu wa janga la COVID-19 duniani. 

Ripoti inataja miongozo ya kuzingatia kama vile kuwepo kwa kanuni za huduma za kujisafi na usafi,  matumizi ya vifaa vya kujikinga,  kunawa na kutakasa mikono na maeneo au vituo vya kunawa mikono kwa maji na sabuni na vyoo visafi. 

Audio Credit
Assumpta Massoi\Loise Wairimu
Sauti
2'53"
Photo Credit
© UNICEF/Vinay Panjwani