Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN4Beirut na mshikamano na wananchi wa Lebanon

UN4Beirut na mshikamano na wananchi wa Lebanon

Pakua

Nchini Lebanon, wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wamezindua kampeni iitwayo Umoja wa Matafa kwa ajili ya Beirut, au UN4Beirut kwa lengo la kuonesha mshikamano na kusaidia watu wa Lebanon kusafisha mitaa ya mji huo mkuu uliosambaratishwa na mlipuko mkubwa wa tarehe 4 mwezi huu wa Agosti. Flora Nducha na maelezo zaidi. 

Wafanyakazi hao pamoja na wale wa kujitolea wamehamasishana wakitumia kauli mbiu yao Umoja wa Mataifa kwa Beirut ili kusafisha mitaa ya mji huo ambamo wamekuwa wakifanyia kazi. 

Nazih Yacoub, mwenyekiti wa chama cha kikanda cha wafanyakazi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, anasema kuwa, 

“Tuko hapa, sote Umoja wa Mataifa, familia moja, timu moja kusaidia kusafisha jiji, jiji ambalo sote tunalipenda, jiji ambalo tunafanyia kazi, tunalipenda hili jiji na hiki ndio kidogo tunachoweza kuifanyia Lebanon na watu wake.” 

Wakiwa wamevalia kofia, barakoa na wengine wamebeba mafagio, ndoo na mifuko ya kubebea taka, wafanyakazi hao wa mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa kutoka maeneo mbalimbali nchini Lebanon wameokota taka, viwe ni vioo , taka ngumu na hata vifusi vilivyofunika mitaa ya Beirut baada ya mlipuko uliosababisha vifo vya watu zaidi ya 200 na wengine zaidi ya 6000 walijeruhiwa huku watu wengine mamia ya maelfu wakisalia bila makazi. 

Lamis Daoud ni afisa kutoka shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR ambaye anasema kuwa, “leo tumeona uharibifu mkubwa. Ni ajabu kuona jinsi taswira ya maisha ya watu ikiwa imesambaratishwa mitaani.” 

Hata hivyo kwa wakazi wa Beirut ambao bado wako na machungu ya kuondokewa na wapendwa wao na wengine bado hawajulikani waliko, kuna matumaini ya kurejea mji wao katika hali ya kawaida kama asemavyo Haidar Fahs, afisa wa kikosi cha mpito cha Umoja wa Mataifa nchini Lebanon, UNFIL. 

"Mimi ni mlebanon ambaye nimekuwa nikitembelea eneo hili. Kuona jinsi mlipuko umeharibu, imekuwa ni hisia kubwa kwangu, kuna wakati nataka kulia kwa sababu nilikuwa nakuja eneo hili kutembea kwenye mitaa. Idadi ya nyumba zilizoharibiwa, maana ya kihistoria ya maeneo mengi imeharibiwa. Inanipa hisia na kunikumbusha kuwa vita ambavyo Lebanon imekumbana navyo. Lakini inanipatia matumaini pale ninapoona watu wakishirikiana, wakisaidiana, ya kwamba tutarejea katika hali bora zaidi kuliko awali.” 

Audio Credit
Assumpta Massoi\Flora Nducha
Audio Duration
2'33"
Photo Credit
© UNICEF/Pasqual Gorriz/UN