Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Waliokufa katika mlipuko Beirut ni pamoja na wakimbizi 34: UNHCR

Waliokufa katika mlipuko Beirut ni pamoja na wakimbizi 34: UNHCR

Pakua

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, limesema limeshtushwa na taarifa kwamba miongoni mwa watu zaidi ya 200 waliopoteza misha kwenye mlipuko mkubwa wa Beirut uliotokea Agosti 4 nchini Lebanon wanajumuisha angalau wakimbizi 34 hadi sasa. Flora Nducha na taarifa zaidi 

Akizungumza na waandishi wa Habari mjini Geneva Uswisi hii leo kwa njia ya video msemaji wa UNHCR Babar Baloch amesema shirika lao bado linathibitisha taarifa hizo hasa ukizingatia kwamba kuna idadi kubwa ya wakimbizi wanaoishi mjini Beiruti na wanahofia idadi ya watu waliopoteza maisha huenda ikapanda zaidi na kuongeza kwamba kutokana na taarifa walizonazo "Wakimbizi 7 bado hawajulikani walipo hadi sasa, wengine 124 wamejeruhiwa katika mlipuko huo na 20 kati yao wamejeruhiwa vibaya.” 

Amesema UNHCR inaendelea kushirikiana kwa karibu na timu za uokozi na wadau wengine wa misaada ya kibinadamu kutambua waathirika na kiwango cha msaada unaohitajika ili kuzisaidia familia zilizopoteza wapendwa wao, na msaada huo ni pamoja na ushauri nasaha, fedha za dharura na kusaidia katika mipango ya mazishi. 

Bwana Baloch amesisitiza kuwa  “Mlipuko umemuathiri kila mtu bila kujali utaifa au hadhi yake, hatua zetu za haraka za kibinadamu kwa ajii ya mlipuko huo zinajumuisha jamii nzima ikiwemo Walebanon, wakimbizi na wafanyakazi wahamiaji. zinajikita kwa wale walio hatarini zaidi katika jamii na ni katika nyanja mbili malazi na ulinzi.” 

UNHCR inakusanya dola milioni 12 inazohitaji kwa hatua za haraka ili kusaidia familia zilizoathirika zaidi Beiruti na fedha hizo zinajumuisha dola milioni 9.6 kwa ajili ya kutoa malazi na dola milioni 2.44 kwa ajili ya shughuli za ulinzi kwa kipindi cha miezi 6 ijayo. 

Mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa likiwemo la kuratibu misaada ya kibinadamu OCHA, la kuhudumia watoto UNICEF, la afya WHO na la mpango wa chakula duniani WFP yote yameungana na mashirika mengine ya misaada ya kibinadamu na yanaendelea kufanya kila liwezekanalo kusaidia katika mahitaji ya dharura ya maelfu kwa maelfu ya watu walioathirika na mlipuko huo wa Beiruti. 

 

Audio Credit
Assumpta Massoi\Flora Nducha
Sauti
2'17"
Photo Credit
© UNOCHA