Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yaendelea na juhudi za kuokoa maisha Beirut

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yaendelea na juhudi za kuokoa maisha Beirut

Pakua

Ikiwa leo ni siku ya saba tangu kutokea mlipuko mkubwa katika mji mkuu wa Lebanon, Beirut, Umoja wa Mataifa kupitia mashirika yake umeendelea kufanya kila juhudi za kuokoa maisha na kurejesha hali ya kawaida katika mji huo ambao ni kiini cha maisha ya nchi hiyo iliyoko  mashariki ya kati.

Mlipuko huo ambao ulitokea wiki iliyopita, Jumanne jioni na kuwaua takribani watu 160, kuwajeruhi maelfu na mamia wengine bado hawafahamiki waliko, umeyafanya mashirika ya Umoja wa Mataifa kufanya kila namna kusaidia kuokoa maisha.  

Kwa mujibu wa makadirio ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF huenda kufikia watoto hadi 100,000 wakawa miongoni mwa ambao makazi yao yamebomolewa na kuharibiwa na mlipuko wa Beirut. UNICEF ina wasiwasi kuwa watoto wengi wamepata kiwewe na wamesalia katika mshituko.  

Kwa mujibu wa taarifa za hivi karibuni, kuna ripoti kadhaa za watoto ambao wametenganishwa na wanafamilia wao, baadhi yao wakiwa bado hawafahamiki waliko. “Takribani vituo 12 vya afya, vituo vya kujifungulia, vya chanjo na vile vya kuwahifadhi watoto baada ya kuzaliwa, vimeharibiwa na hivyo kuathiri huduma kwa takribani watu 120,000.” Inasema UNICEF. 

Hospitali ya watoto katika eneo la Karatina ambayo ilikuwa na kitengo maalumu cha kutibu watoto wachanga walioko katika hali mbaya, imeharibiwa. Hospitali ambazo zimesalia zikifanya kazi zimeelemewa na zimeishiwa dawa muhimu.  

Wanajamii wakisafisha mazingira baada ya mlipuko uliotokea eneo la Gemmayze, huko Beirut, Lebanon.
© UNICEF/Ramzi Haidar
Wanajamii wakisafisha mazingira baada ya mlipuko uliotokea eneo la Gemmayze, huko Beirut, Lebanon.

UNICEF inasema, “vyumba vya baridi vitano kati ya saba vya kuhifadhia chanjo ambavyo vinadhaminiwa na UNICEF vimeharibiwa na mlipuko na hivyo kuathiri mpango wa chanjo. Wakati tathmini bado inaendelea, shule nyingi zimeripotiwa kuharibiwa mjini Beirut pamoja na maeneo ya jirani.” 

Shirika hilo la kuhudumia watoto linashirikiana na wadau kuongeza msaada kwa watoto walioathirika, pamoja na familia zao ili kushughulikia mahitaji ya haraka.  

Wakati huo huo shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO nalo linapambana kuhakisha watu wanapata mahitaji ya huduma za kiafya huku shirika Umoja wa Mataifa la idadi ya watu duniani, UNFPA pia linachangia tathmini ya pamoja ya hospitali na vituo vya huduma ya afya ya msingi ili kuona kiwango cha uharibifu wa afya ya kijinsia na uzazi.  

Taarifa iliyotolewa na UNFPA inasema juhudi kwa sasa zinalenga ununuzi wa vifaa vya matibabu na vifaa kwa idara za uzazi na vituo vya afya vilivyoathirika, pamoja na kusaidia utoaji 25% wa mahitaji ya manunuzi yaliyotathiminiwa na WHO kwa ajili ya miezi sita ijayo.  Vile vile ili kuhakikisha mwendelezo wa huduma, UNFPA itaajiri na kupeleka wafanyakazi wa nyongeza ikiwa ni pamoja na wakunga katika vituo vya afya kwa mujibu wa ombi la Wizara ya Afya ya Umma ya Lebanon. 

Audio Credit
Assumpta Massoi\Flora Nducha
Audio Duration
1'48"
Photo Credit
© UNICEF/Ramzi Haidar