Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Misaada yaelekezwa Beirut, OHCHR yataka uchunguzi wa kina

Misaada yaelekezwa Beirut, OHCHR yataka uchunguzi wa kina

Pakua

Siku tatu tangu mlipuko mkubwa kusababisha vifo, majeruhi na uharibifu mkubwa kwenye mji mkuu wa Lebanon, Beirut, mashirika ya Umoja wa Mataifa na wadau wake wanapeleka misaada ya hali na mali huku ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa ikitaka uchunguzi wa kina na mamlaka ya thabiti ili kuepusha hali kama hiyo isitokee tena. Assumpta Massoi na ripoti kamili. 

Jiji la Beirut na viunga vyake, bandari ya Beirut vimesalia magofu, vifusi vya mabaki ya majengo vikiwa ndio taswira halisi ya sasa. 

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF linakadiria kuwa takribani watoto 100,000 ni miongoni mwa ambao nyumba zao zimeharibiwa au kusambaratishwa, huku nyumba nyingine zikiwa hazina huduma za kutosha za maji na umeme, au hazina kabisa huduma hiyo, mustakabali wa watoto ukiwa mashakani. 

UNHCR kwa upande wake ina hofu kuwa wakimbizi waliokuwa wanaishi mjini Beirut, ni miongoni mwa manusuru kwa hivyo hivi sasa wanashirikiana na wadau kuona jinsi ya kusaidia harakati za serikali ya Lebanon na maeneo muhimu ya usaidizi ni malazi, afya na ulinzi. 

Kwa upande wake ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR, imesema tukio la Jumanne ni kengele kwa jamii ya kimataifa kuongeza usaidizi wake kwa Lebanon na watu wake, ikisema msaada zaidi utaepusha kupotezwa zaidi kwa maisha ya watu. 

Msemaji wa OHCHR Rupert Colville amesema kuwa, "Leo hii kila mlebanon anawaza ni vipi wataendeleza maisha yao katikati ya majanga matatu; janga la kiuchumi na kijamii, COVID-19 na sasa mlipuko uliosababishwa na Amoniamu Naitrate.” 

OHCHR imetaka uchunguzi wa kina na huru kuhusu sababu za kuendelea kuwepo kwa shehena hiyo ya kemikali ya Amoniamu Naitrate itumikayo kama mbolea na kilipuzi. “Baadhi ya mambo yameshasemwa kwa kina na tunafahamu kemikali hiyo ilipotoka, na ilivyofika pale na kadhalika na swali kubwa ni kwa nini ilibakia kwenye bohari kwa miaka 7?” 

Audio Credit
Anold Kayanda\ Assumpta Massoi
Audio Duration
2'10"
Photo Credit
© UNOCHA