Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

MINUSCA yapigia chepuo azma ya CAR ya kuondoa machungu magerezani

MINUSCA yapigia chepuo azma ya CAR ya kuondoa machungu magerezani

Pakua

Wanawake wafungwa katika gereza la Bimbo lililoko kilometa takribani 10 kutoka mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, Bangui watanufaika na mradi wa ujumuishwaji katika jamii unaotekelezwa na ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini  humo, MINUSCA. Flora Nducha na maelezo zaidi. 

Mradi huo wa MINUSCA wa kusaidia wafungwa kutangamana vema katika jamii umewezesha makabidhiano ya vifaa kwa gereza hilo, vifaa ambavyo ni pamoja na vyerehani 6, mashine mbili za kufyatulia vifungo, pasi za kunyooshea nguo na vitabu vya elimu ya watu wazima. 

MINUSCA inasema msaada huo kupitia kitengo chake cha huduma za sheria na magereza kinalenga kuimarisha miradi ya ujumuishaji katika jamii kwa minajili ya kupunguza kiwango cha wafungwa wasiojua kusoma na kuandika na pia kufanikisha mipango ya kujumuika na jamii zao wakiachiliwa huru. 

Mkurugenzi wa utawala katika gereza la Bimbo, Dieudonné Mbolinanguera akizungumza wakati wa kupokea vifaa hivyo amesema Suala la kujengea uwezo wafungwa ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa CAR wa ujumuishaji wafungwa nchini humo kuanzia mwaka 2017 hadi 2022 na kwamba,  "Tatizo la ujumuishwaji wa kijamii ni moja ya malengo yetu dhahiri ya sera ya usimamizi ya ujumuishwaji wa kijamii. Unaona katika sheria yetu namba 2003 inazungumzia magereza kuwa maeneo ya kiutu.” Akifafanua lengo la MINUSCA, Amina Diakhate, afisa magereza wa ujumbe huo amesema kuwa, “Tuna malengo mawili, lengo la usalama na lengo la kuandaa wafungwa kwa kujumuika vyema na jamii kwa hiyo mradi huo uko kwenye eneo hilo.” 

Akizungumza baada ya makabidhiano ya vifaa hivyo vyenye thamani ya zaidi ya dola 9,700, mmoja wa wanawake wafungwa 21 watakaonufaika na mradi huo amesema kwa miaka mitano ambayo amekuwa gerezani amesahamu kila kitu.  

Hata hivyo amesema anashukuru kwa neema ya Mungu wamepokea msaada na watapatiwa mafunzo ambayo yatamuimarisha na hatimaye akitoka anaweza kusaidia familia yake. 

 

Audio Credit
Assumpta Massoi\Flora Nducha
Sauti
2'13"
Photo Credit
MINUSCA/Hervé Serefio