Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ajabu kubwa, miaka 75 tangu Hiroshima na Nagasaki bado nchi zinalea nyuklia- Guterres

Ajabu kubwa, miaka 75 tangu Hiroshima na Nagasaki bado nchi zinalea nyuklia- Guterres

Pakua

Ikiwa leo ni miaka 75 tangu Marekani iangushe bomu la atomiki kwenye eneo la Hiroshima nchini Japan, Katibu Mkuu wa Umoja waMataifa Antonio Guterres amesema njia pekee ya kuondokana na tishio la nyuklia ni kutokomeza silaha za nyuklia. Loise Wairimu na ripoti kamili. 

Katika ujumbe wake wa siku hii ya leo, Katibu Mkuu amesema amezingatia ukweli kwamba miaka 75 iliiyopita, silaha moja ya nyuklia ilileta vifo na uharibifu katika mji huo. "Madhara yake yako hadi leo. Mji na watu wake, hata hivyo wamechagua kutotambuliwa kwa majanga bali kwa mnepo, maridhiano na matumaini. Kama wachechemuzi wa kipekee katika utokomezaji wa silaha za nyuklia, Hibakusha wamebadili janga lao kuwa sauti ya pamoja ya ustawi wa ubinadamu.” 

Katibu Mkuu amekumbusha kuwa tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa, mwaka 1945, chombo hicho kilitambua umuhimu wa kutokomeza silaha hizo kwa kuwa ni  kipindi hicho hicho mabomu yalisambaratisha Hiroshima na Nagasaki. 

Cha ajabu hadi leo lengo hilo bado halijafikiwa, amesema Katibu Mkuu akiongeza kuwa, “miaka 75 ni mingi mno kwa kutotambua kuwa umiliki wa silaha za nyuklia unasambaratisha badala ya kuimarisha usalama.  

Amesema leo hii dunia bila silaha za nyuklia inaonekana kuponyoka na wamiliki wa nyuklia wanazidi kuimarisha makombora yao. “Natoa wito kwa serikali zirejee katika dira ya pamoja na mwelekeo wa kutokomeza kabisa silaha za nyuklia. Sasa ni wakati wa mazungumzo, kuweka mikakati ya kujengeana imani, kupunguza ukubwa wa silaha za nyuklia na zaidi ya yote kujizuia kuzitumia.” 

Katibu Mkuu amekumbusha kuwa kila mtu ana jukumu katika kutokomeza silaha za nyuklia akisema vijana na mashirika ya kiraia wameonesha  nguvu yao mara kwa mara katika kuunga mkono kutokomeza silaha za nyuklia akisema wapatiwe fursa ili wapaze sauti zao. 

Amesema Umoja wa Mataifa kwa upande wake utaendelea kufanya kazi na wale wote wanaosaka kufanikisha lengo la pamoja la dunia bila silaha za nyuklia. 

 

Audio Credit
Assumpta Massoi\Loise Wairimu
Audio Duration
1'39"
Photo Credit
UN /Nagasaki International